TEMESA YAZIDAI MILIONI 500 TAASISI MKOANI RUKWA

News Image

Posted On: November 22, 2023

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) unazidai zaidi ya shilingi Milioni 500 Taasisi za Serikali Mkoani Rukwa ambazo zinapatiwa huduma na Wakala huo. Hayo yamebainishwa Tarehe 21 Novemba 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Charles Makongoro Nyerere wakati alipokuwa akizungumza kwenye Kikao na wadau wanaotumia huduma za Wakala huo wakiwemo wauzaji wa vipuri, wasambazaji wa vilainishi, wasimamizi wa gereji binafsi pamoja na wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali Mkoani Rukwa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Nazareti ulioko Mkoani humo.

MheMakongoro amesema sambamba na maboresho ambayo Wakala unaendelea kuyafanya katika karakana zake kote nchini ikiwemo ujenzi wa karakana mpya, ukarabati wa karakana za zamani pamoja na ununuzi wa vitendea kazi vipya, lakini ili TEMESA iweze kutoa huduma zilizo endelevu, ni lazima Taasisi zote za Serikali Mkoani humo kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati.

‘’Sasa tunambiwa Mkoa wa Rukwa, tunadaiwa na TEMESA Milioni 500, unakuwa na gari lako unalipeleka halafu hulipii, inakuja bajeti mpya unapewa fungu la fedha za kulipia matengenezo, hulipi halafu baadae unaanza kulamu, tutaiua TEMESA, tutakaa tunalaumu wakati kulipa hatulipi we unataka huduma halafu kulipa hulipi.’’ Amesema Mhe. Makongoro na kuongeza kuwa changamoto hiyo ni kubwa na inaurudisha nyuma sana Wakala kutokana na kutokulipwa kwa wakati.

Awali akizungumza na wadau hao mapema asubuhi, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bi. Josephine Matiro amesema Mkoa wa Rukwa ni Mkoa wa 17 ambao Wakala umefanya kikao na wadau wake mpaka sasa kati ya Mikoa 26 ambayo Wakala una ofisi zake za karakana. Amesema Wakala huo umejitathmini na kuona changamoto ambazo uko nazo na kama Taasisi nyingine za Kiserikali ukaamua kuchukua hatua ili kufanya mabadiliko na maboresho makubwa.

‘’Tumejitathimini tukaona mapungufu yetu, changamoto zetu na tumeanza kuzifanyia marekebisho, lakini tukasema tusiwe wabinafsi, twende huko ambako tunatoa huduma kwasababu lengo letu ni kutoa huduma yenye tija inayowapendeza wale ambao tunawapa huduma, ambao ndio hawa tumewaalika humu ndani leo, twende tukawasikie wanasemaje, huduma zetu je, zimeanza kurekebishika? Amesema Matiro na kuongeza kuwa TEMESA imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu huku akisisitiza kuwa tayari kuna mabadiliko yameanza kuonekana katika Mikoa tofauti ikiwemo mabadiliko ya kifikra, kiutendaji pamoja na kiuwezo.

Naye, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Hassan Karonda akizungumza katika kikao hicho amesema tayari kuna hatua za mwanzo ambazo Wakala huo umezifanya kwa haraka ili kuwafanya wateja wake waweze kuridhika na huduma wanazotoa ambapo amesema changamoto zilizokuwepo kubwa ni ucheleweshaji wa matengenezo na gharama za matengenezo ambapo amesema tayari Wakala umerekebisha tatizo hilo.

‘’Tumekuja na utaratibu wa kuingia mikataba ya moja kwa moja na wazabuni Zaidi ya 56 nchi nzima kwa ajili ya kusambaza vipuri kwa TEMESA yote, kwahiyo hiyo inafupisha ule ucheleweshaji kwakuwa zile taratibu za ununuzi zinakuwa zimefanywa kwa wakati mmoja, kwahiyo hii inatusaidia kufupisha ule muda,’’ amesema Mhandisi Karonda huku akisisitiza kwamba mzabuni yoyote ambaye atakwenda kinyume na mkataba unavyosema ikiwemo kuleta kipuri ambacho sio halisi basi atashitakiwa kwa mujibu wa mkataba na atatakiwa kulipia kifaa husika ili kiweze kubadilishwa kwenye gari husika.