​WAAJIRIWA WAPYA TEMESA WAFUNDWA

News Image

Posted On: September 04, 2024

Waajiriwa wapya wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA kutoka kada za Masijala, Ununuzi, Ufundi, Umeme, Mitambo na Ufundi wa vivuko wamepatiwa mafunzo elekezi yenye lengo la kuwaandaa kufanya kazi kwa weledi na kufuata misingi ya Kiutumishi.


Akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa mikutano wa TEMESA Makao Makuu jijini Dodoma Septemba 06, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda amewataka waajiriwa hao kutimiza majukumu yao kwa ufanisi ili kuleta chachu ya mabadiliko TEMESA.

Mhandisi Karonda amewakumbusha watumishi hao kuwa, wanatakiwa kutimiza dhamana walizopewa kwa uadilifu na kupata kazi serikalini kusiwe sababu ya kutokutimiza majukumu yao huku akiwasihi wawe mfano wa kuigwa kwa jamii zinazowazunguka.

“Kuna dhamana ambayo umepewa lazima uitimize usijesema nimapata sasa cheki namba ukasema nimepatia, huko mitaani unatakiwa uwe mfano mzuri wa wewe kufanya kazi serikalini” amesisitiza Mha. Karonda.

Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Bi. Josephine Matiro amewakaribisha watumishi wapya na kuwaasa kufanya kazi kwa bidii, uaminifu, umoja, mshikamano na heshima kwa viongozi wao.

“Mimi niwakaribishe TEMESA, TEMESA ni kitu kikubwa na tuko kwenye mkakati wa mabadiliko ya kiutendaji na mengine yanasubiri uthibitisho wa wizara na juu zaidi ili tuweze fanya kazi kwa weledi na tubadilike” alisisitiza Bi. Matiro.

Mafunzo hayo wezeshi kwawatumishi wapya yanafanyika kwa siku tatu na yanatarajiwa kukamilika siku ya Tarehe 4 Septemba, 2024.