WATUMISHI TEMESA MWANZA WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO WA KIDIGITALI WA MUM
Posted On: April 22, 2025
Watumishi wa karakana ya TEMESA Mkoa wa Mwanza wamepatiwa mafunzo maalumu kuhusu namna ya kutumia mfumo mpya wa kidigitali wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo MUM.
Mafunzo hayo yamefanyika katika karakana ya TEMESA Mkoa wa Mwanza iliyoko eneo la Igogo na kuendeshwa na Mkufunzi wa Mfumo huo ambae pia ni Meneja wa kikosi cha Umeme, Mhandisi Pongeza Semakuwa na kuhudhuriwa na Meneja wa TEMESA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Frank J Msyangi pamoja na watumishi wa TEMESA kutoka mkoa wa Mwanza.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhandisi Semakuwa amesema mfumo huo utawezesha TEMESA kufuatilia kazi za matengenezo kwa wakati, kuweka kumbukumbu sahihi za majengo, na kutoa taarifa za kiutendaji zinazosaidia maamuzi sahihi.
“Mfumo huu unaleta uwazi katika huduma ambazo taasisi inatoa kwa taasisi nyingine za serikali lakini pia inaleta uwajibikaji kwa watumishi kwa sababu mfumo huu umejumuisha vipengele muhimu vitakavyosaidia watumishi kuingia kwenye mfumo na kutekeleza majukumu yao”amesema mhandisi Pongeza.
Kwa upande wake, Meneja wa TEMESA Mwanza ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuifanyia TEMESA mabadiliko na kutoa rai kwa watumishi waliopatiwa mafunzo hayo kuhakikisha wanayatumia kwa ufanisi na kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya mfumo huo katika taasisi.
“Naishukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa kutuanzishia mfumo ambao umeweza kuturahisishia kutoa huduma bora kwa wananchi na tunashukuru tumeanza kupata mfunzo ya ndani kwq watumishi ili kuwa na mwamko wa mfumo huu wa MUM”
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi. Salome Kilowoko kutoka Idara ya Manunuzi, amesema mfumo wa MUM umewasaidia kufanya kazi kwa haraka na wakati sahihi ukilinganisha na kipindi cha nyuma.