BODI YA USHAURI TEMESA YARIDHISHWA NA KASI UJENZI NA UKARABATI VIVUKO
Posted On: April 17, 2023
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA Mhandisi Deogratias Nyanda, wajumbe wa bodi hiyo pamoja na menejimenti ya Wakala chini ya Mtendaji Mkuu Lazaro Kilahala, leo wamefanya ziara Mkoani Mwanza kukagua ujenzi wa vivuko vipya na ukarabati wa vivuko unaoendelea Mkoani humo katika yadi ya Songoro iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Deogratias Nyanda amesema bodi hiyo imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa vivuko vipya vinne ambavyo vinagharimu kiasi cha shilingi bilioni 17 ambavyo vitaenda kutoa huduma katika maeneo yaBwiro Bukondo, Kisorya Rugezi, Nyakaliro Kome na Ijinga Kahangala.
Mhandisi Nyanda amesema baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko hivyo vipya pamoja na wajumbe wa Bodi hiyo, wana uhakika kuwa vivuko hivyo vitakamilika kwa wakati kwakuwa Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo kwa mkandarasi Songoro Marine.
‘’Wajibu wa Bodi ni kuhakikisha kwamba tunafanya kwa uwezo wetu upande wa ushauri, TEMESA kwa upande wao ni utoa huduma kwa Watanzania kwa niaba ya Serikali, kwahiyo sisi tuna matumaini makubwa kwamba sasa kazi itaenda vizuri kwasababu tumeshajionea wenyewe na mkandarasi ametuhakikishia kwamba vifaa vinavotakiwa vipo vimeshafika,’’ amesema Mwenyekiti.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA Lazaro Kilahala amesema miradi hiyo ya ujenzi wa vivuko vipya vinne na ukarabati wa vivuko vya MV.MISUNGWI, MV. MARA, MV. UJENZI, MV. KILOMBERO NA MV. NYERERE kwa ujumla wake, mikataba yake inafikia thamani ya takribani shilingi Bilioni 60.
‘’Viko vivuko mbalimbali vinavyojengwa na kukarabatiwa katika maeneo tofauti, vivuko ambavyo ni vipya vinaendelea kujengwa hapa, tuna kivuko kile cha Kisorya Rugezi, Bwiro Bukondo, Ijinga Kahangala na Nyakaliro Kome, kwahiyo kilichotuleta hapa ni hicho na kwakweli tumeridhika na kasi ya ujenzi inayoendelea, tunaendelea kuishukuru Serikali yetu kwa kuendelea kuwezesha haya, kazi inakwenda vizuri kwasababu na malipo yanafanyika kwa wakati.’’ Amesema Mtendaji Mkuu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro inayosimamia ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo Major Songoro, akizungumza katika ziara hiyo amesema miradi hiyo mipya inayotekelezwa na ile ya ukarabati wa vivuko imefikia katika hatua mbalimbali.
‘’Tuko kwenye hatua za (Hull) hii ni sehemu ya chini ya chombo ambayo inakaa chini ya maji, hivi vivuko vyote viko katika hatua hiyo, tunatarajia kwenye mwezi wa nane vitaanza kukamilika.’’ Alisema Songoro.
Mapema asubuhi, wajumbe hao walipata wasaa wa kukagua karakana ya matengenezo ya magari iliyopo maeneo ya Igoma Mkoani humo ambapo walikagua ukarabati unaoendelea wa karakana hiyo.