MENEJIMENTI YA TEMESA YAWASILISHA TAARIFA YA UTENDAJI KWA BODI YA USHAURI

News Image

Posted On: July 04, 2026

Menejimenti ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) leo tarehe 4 Julai, 2026, imekutana na Bodi ya Ushauri ya Wakala katika kikao maalum cha kujadili utendaji wa taasisi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu ya Wakala.

Katika kikao hicho, Menejimenti iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikieleza mafanikio yaliyopatikana katika utoaji wa huduma za ufundi, maendeleo ya miradi ya kimkakati, matumizi ya teknolojia za kidijitali, pamoja na hatua zilizochukuliwa kuboresha ufanisi wa huduma kwa wateja na taasisi za Serikali.

Aidha, kikao kilijadili changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu ya Wakala na kuweka mikakati ya kuendelea kuimarisha utendaji, kuongeza tija, kuboresha utoaji wa huduma na kuhakikisha TEMESA inaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia viwango vya ubora, uwazi na uwajibikaji.

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri wa Wakala wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Andrew W. Massawe, wameipongeza Menejimenti kwa mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi hicho na kutoa maelekezo na ushauri wa kitaalamu utakaoiwezesha TEMESA kuendelea kuboresha huduma zake na kuchangia kwa ufanisi zaidi maendeleo ya Taifa.

TEMESA inaendelea kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Ushauri pamoja na wadau mbalimbali katika kuendeleza ubunifu, kuimarisha mifumo ya utendaji na kuhakikisha wananchi na taasisi za Serikali wanapata huduma bora, salama na zenye kuaminika.