MKURUGENZI WA HUDUMA ZA UFUNDI ATEMBELEA BANDA LA TEMESA KATIKA MAONESHO YA 50 YA SABASABA
Posted On: July 04, 2026
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Mha. Hassan H. Karonda, tarehe 3 Julai 2026, ametembelea banda la TEMESA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza na watumishi katika banda la TEMESA, Mha. Karonda kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TEMESA Kheri Mahimbali amewapongeza watumishi wanaoshiriki maonesho hayo kwa kujituma na kutoa huduma bora kwa wananchi, huku akiwahimiza kuendelea kudumisha weledi, ubunifu na uwajibikaji katika utoaji wa huduma.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuitangaza TEMESA na kuwahudumia wananchi kwa weledi na moyo wa kujituma. Maonesho haya ni jukwaa muhimu la kuonesha uwezo wetu, kusikiliza maoni ya wananchi na kuendelea kuboresha huduma zetu ili ziendane na matarajio ya Watanzania.”amesema Mha. Karonda.
Aidha, Mha. Karonda amesema ushiriki wa TEMESA katika maonesho hayo unaendelea kutoa fursa kwa wananchi kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TEMESA, zikiwemo huduma za vivuko, matengenezo ya magari, huduma za umeme na elektroniki, ushauri wa kihandisi pamoja na mifumo ya kidijitali.
Maonesho hayo yamefunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwa ameambatana na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji , Mhe. Daniel Frasisco Chapo.