MENEJA KANDA TEMESA AWATOA HOFU WAKAZI WA IZUMACHELI KUHUSU KIVUKO CHA MV. TEGEMEO

News Image

Posted On: May 09, 2023

Meneja wa Vivuko Kanda ya Ziwa na Magharibi Mhandisi Vitalis Bilauri amesema kuwa Serikali kwa sasa haina mpango wa kusitisha safari za kivuko cha MV. TEGEMEO kwenda kwenye kisiwa cha Izumacheli Wilayani Geita Vijijini hadi hapo kivuko mbadala kitakapopatikana. Mhandisi Bilauri ametoa ufafanuzi huo wakati akizungumza na mwandishi wa Televisheni ya Taifa TBC kufuatia hofu ya wakazi wa kisiwa hicho kuwa kivuko hicho hakitatoa huduma ya uchukuzi kati ya eneo la Kahunda Wilayani Sengerema na Nkome Wilayani Geita kupitia kisiwa cha Maisome na Izumacheli kutokana na kujiendesha kwa hasara.

Mhandisi Bilauri amesema kivuko cha MV.TEGEMEO kinafanya huduma zake katika kisiwa cha Izumacheli kwa majaribio.’’Tumefanya haya majaribio ya kuongeza ruti kwenda Izumacheli lakini mtihani tuliokutana nao ni kivuko kuanza kujiendesha kwa hasara,Serikali haina mpango wa kusitisha safari za kivuko hicho, kuna taratibu ambazo tunazifanya za kuona kama tukifanikisha kupata kivuko kingine mbadala, ambacho ni kidogo ambacho hata uwezo wake (tani) ni ndogo kulinganisha na MV. TEGEMEO, kile ambacho kinaweza kikalingana na mazingira ya pale itakuwa ni bora zaidi na hizo ni jitihada ambazo tunaendelea kuzifanya kila siku. Amesema Mhandisi Bilauri.

Inaaminika kuwa hali usafiri wa abiria na mizigo imeimarika katika kisiwa cha Izumacheli kilichopo katika Ziwa Viktoria Wilayani Geita baada ya kivuko MV. TEGEMEO kuanza kutoa huduma za uchukuzi kwenye kisiwa hicho chenye zaidi ya wakazi elfu tano.

Siku kadhaa baada ya kivuko hicho kuanza kutoa huduma, wakazi wa Kisiwa cha Izumacheli wamekumbwa na hofu na wasiwasi kutokana na hapo awali kutozwa nauli kubwa ya shilingi 1500 kutoka kata ya Izumacheli kwenda Nkome kwa kutumia mitumbwi midogo ya mbao ya wavuvi wa maeneo hayo tofauti na gharama ya nauli ya shilingi 800 ambayo Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA umekuwa ukiwatoza kwa kutumia kivuko cha MV.TEGEMEO.

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA, imeombwa na wananchi wa maeneo hayo kutositisha safari za kivuko hicho kwa kuwa usafiri uliopo maeneo hayo sio wa uhakika na salama kwa abiria hao na mali zao lakini pia hauwafikishi kwa wakati kwenye maeneo wanakokwenda. Wananchi hao wameiomba mamlaka kutilia mkazo suala hilo la usafiri na kutowarudisha nyuma kuanza tena kutumia usafiri wa mitumbwi na boti ndogo ndogo kama waliyokuwa wakitumia hapo awali ambayo haina usalama wa uhakika.