TEMESA INATEKELEZA MIRADI MIKUBWA YA UMEME BARIADI MKOANI SIMIYU

News Image

Posted On: August 30, 2022

Ofisi ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Simiyu inaendelea na miradi ya kusimika mifumo ya Umeme, Elektroniki, Viyoyozi na Viashiria moto katika Halmashauri ya mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, miradi hiyo inahusisha kusimika mifumo ya majokofu na viyoyozi katika jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu ambapo wanashirikiana kufanya mradi huo na ofisi ya Kikosi cha Umeme (TEMESA Dar es Salaam). Mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 400.

Aidha, Kikosi hicho pia kinasimika mifumo ya umeme na viashiria moto katika jengo la dharura na wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika hopitali hiyo, mradi uliogharimu shilingi milioni 177.5, vilevile ofisi ya TEMESA Simiyu inashiriki kusimika mifumo ya umeme na viashiria moto katika jengo la Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ofisi ya TEMESA Mkoani Simiyu pia inasimika mifumo ya umeme katika nyumba mpya inayojengwa ya kuishi mtumishi, pia kikosi hicho kinasimika mifumo ya umeme katika nyumba ya mtumishi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa pamoja na kusimika mifumo ya umeme katika nyumba tatu za watumishi wa Serikali Mkoani humo.

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kupitia Kikosi cha Umeme na Ofisi ya Wakala huo Mkoa wa Simiyu imetoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, Halmashauri ya Mji wa Bariadi pamoja na Wakala wa Majengo nchini (TBA) kwa kuendelea kuiamini na kuipatia fedha za kutekelea miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotokelezwa hapa nchini na kuahidi kuisimamia miradi hiyo kwa ufanisi huku ikitoa rai kwa taasisi zingine za Serikali na binafsi kuendelea kuuamini wakala huo na kuupatia kazi kwakua Wakala umejipanga kutekeleza miradi hiyo kwa viwango bora pamoja na kutoa huduma bora kwa washitiri wake wakati wote.