TEMESA YAJA NA ‘MUM’, MFUMO UTAKAOBORESHA HUDUMA KWA WATEJA KUPITIA KARAKANA ZAO

News Image

Posted On: March 15, 2025

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), imefanya kikao cha Mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Matengenezo (MUM) Kwa Washitiri na Wadau wa Karakana Teule Kutoka katika sekta na taasisi mbalimbali nchini ili kuboresha mfumo wake wa utoaji huduma, mafunzo hayo yamefanyika leo Machi 15, 2025 katika ofisi za Wakala huo jijini Dodoma.

Lengo la mafunzo hayo ni kutoa muongozo kwa washitiri na wadau kuhusu namna ya kutumia mfumo huo ili kurahisisha mawasiliano baina ya TEMESA na Taasisi Nunuzi tofauti na hapo kabla ambapo ilichukua muda mrefu.

Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, Meneja wa TEMESA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Greyson Maleko amesema kuwa, serikali imeelekeza mabadiliko hayo makubwa ya Kitaasisi ili kuiboresha TEMESA kiutendaji.

“Tunahitaji kuwa na kanzi data ya magari yote ya Serikali na taarifa zake za matengenezo, kama ambavyo hapo awali taarifa hizo na kumbukumbu zilikua zinapatikana kwenye majalada, hilo lilileta shida kwenye kupata huduma kwa wakati kwa vyombo tunavyo vihudumia.

“Taasisi mbalimbali zaidi ya sabini zimehudhuria mafunzo haya yenye lengo la kurahisisha mfumo wa mawasiliano baina ya TEMESA na Taasisi Nunuzi ili kuanza kuona namna huduma zinavyopokelewa na kufanyiwa kazi na jinsi taarifa nyingi na muhimu za matengenezo ya magari, majenereta, mifumo ya umeme, viyoyozi kwenye majengo ya serikali vinavyoweza kufanyiwa kazi kwa ufanisi.” alisema Maleko.

Pia aliongeza kwa kusema kuwa, Mafunzo haya yatakuwa ni suluhisho kwa ajili ya mfumo ambao unaenda kutatua hilo tatizo la ucheleweshwaji wa huduma hivyo itaongeza ufanisi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mfumo wa MUM Mhandisi Pongeza Semakuwa, Meneja TEMESA Kikosi cha Umeme amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa ndio yanaleta mrejesho wa matumizi ya Mfumo na namna ya ufanisi katika kazi na kuwa itapunguza muda wa utaratibu pale wanapokuja kupatiwa huduma ya matengenezo na wako tayari kupokea maoni ya wadau kwa kulenga kuboresha mfumo ili ukidhi matakwa ya wateja lakini pia Watumishi wa ndani.

Nae, Afisa Usafirishaji Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya, Hakim Joseph ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TEMESA kwa kuletwa kwa mfumo huo kwa sababu utarahisisha shughuli za utoaji huduma.