TEMESA YASIMIKA TAA ZA KUONGOZEA MAGARI UBUNGO FLYOVER, SAM NUJOMA NA SHEKILANGO

News Image

Posted On: April 29, 2021

Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kupitia Kikosi Cha Umeme ambacho kinasimamia kazi za kandarasi za mifumo ya Umeme, Elektroniki, TEHAMA, Viyoyozi pamoja na Usimikaji na matengenezo ya taa za barabarani umesimika taa za kuongozea vyombo vya moto (traffic lights) katika barabara za Shekilango, Sam-Nujoma na Ubungo Interchange jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na mwandishi wetu mapema leo, Meneja wa Kikosi cha Umeme aliyesimamia mradi huo Mhandisi Pongeza Semakuwa amesema mradi huo umekamilika na umeanza kutumika na taa hizo zimesimikwa kwa kutumia fedha za ndani zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‘‘Katika barabara ya Shekilango, taa hizo tumezisimika katika makutano yapatayo matano kwa gharama ya shilingi milioni 700, Katika barabara ya Sam-Nujoma taa hizo tumezisimika katika makutano matatu yaliyopo Mawasiliano tower na Simu 2000 kwa gharama ya shilingi milioni 350, wakati katika makutano ya Ubungo ‘flyover interchange’ kazi hii imefanyika kwa kushirikiana na mkandarasi wa mradi wa daraja hilo kwa gharama ya shilingi milioni 70,’’ alisema Mhandisi Pongeza.