TEMESA SASA MAMBO KIDIGITALI, MALIPO NI KABLA

News Image

Posted On: March 07, 2025

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umetoa wito kwa Taasisi za Umma na Wizara zote za Serikali kuunga mkono Wakala wakati huu ambapo umeanza utaratibu mpya wa malipo kabla (Pre-paid) ambapo mteja analazimika kulipia kabla ya kupatiwa huduma ya matengenezo ya magari, mitambo, makangavuke (majenereta), kazi za umeme, elektroniki, kazi za TEHAMA, vipandio )Lift) na viyoyozi.

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ukarabati wa karakana ya Mkoa ya Dodoma ambayo inafanyiwa ukarabati mkubwa ili kuiongezea ufanisi iweze kutoa huduma katika hali ya ubora.

Mhandisi Karonda amesema Serikali imeridhia TEMESA kuanzia wakati huu itumie mifumo ya kidigitali huku malipo ya huduma husika za matengenezo zilkitakiwa kulipiwa kabla (Pre-paid) ambapo amefafanua ya kwamba mteja anapopata makadirio yake na kuridhia kwenye Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM) ambao unapatikana kupitia tovuti ya mum.temesa.go.tz, mteja atapewa chaguzi tatu, mteja atatakiwa alipe kabla matengenezo ya gari husika hayajaanza au alipe wakati matengenezo yakiwa yanaendelea au matengenezo yatakapokamilika kabla hajachukua gari husika lazima alipie matengenezo hayo ndipo ataruhusiwa kuchukuwa gari husika.

''Nichukue nafasi hii kuwaomba na kuwahimiza wateja wetu mtuunge mkono katika hili na tumetoa maagizo kwa mameneja wetu wa Mikoa kuhakikisha kwamba wanatoa elimu na kuwafundisha wateja wetu kuhusiana na mfumo huu, katika mfumo huu kuna vitu vingi kama nilivosema hizo bei zinakuwa zinajumlishwa na kutolewa kidigitali lakini pia kuna mfumo huu unasaidia kurahisisha kazi na kuokoa muda, vitu vyote vinakuwa vinafanyika kwa muda mfupi na ufanisi wake unakuwa ni wa hali ya juu,'' amesema Mhandisi Karonda na kuongeza kuwa hayo ni maelekezo ya Serikali na TEMESA inatekeleza kwakuwa maelekezo hayo yatasaidia kuleta ufanisi bora wa utendaji kazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA).

Mhandisi Karonda pia ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha maeneo ya ufanyaji kazi ikiwemo karakana kwa kununua vitendea kazi vipya pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya kupeleka mafundi kwenye mafunzo ambayo yanawasaidia mafundi hao kujiongezea ujuzi ili kuendana na teknolojia za kisasa zinazokuja na magari mapya yanayoendelea kutoka mara kwa mara ambapo kwa Mkoa wa Dodoma Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa karakana hiyo na pindi ukarabati huo utakapokamilika karakana hiyo itakuwa ya kisasa na mazingira ya kazi yatakuwa yameboreka kwa kiasi kikubwa na kuwafanya watumishi wajisisike fahari kufanya kazi katika maeneo yanayoonekana vizuri.