MAAFISA RASILIMALI WATU, WAGAVI NA WAHASIBU TEMESA WAPATIWA SEMINA YA KUWAJENGEA UWEZO
Posted On: April 29, 2025
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA umeendesha semina maalum kwa wahasibu, wagavi na maafisa rasilimali watu kutoka vituo mbalimbali vya wakala huo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa TEMESA Makao Makuu na imefunguliwa na Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala.
Akizungumza na watumishi hao wakati akifungua semina hiyo, Mtendaji Mkuu amewataka kuhakikisha kuwa semina hiyo inakuwa chachu ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji, ubunifu sambamba na kuendana na mabadiliko makubwa yanayoendelea kufanyika ndani ya Wakala.
“Katika kipindi hiki cha mageuzi ndani ya TEMESA, tunahitaji watu walio tayari kubadilika, kutumia maarifa yao kikamilifu na kuleta tija katika Taasisi. Mafanikio yetu kama Taasisi yatategemea ubora wa kazi zenu katika maeneo ya fedha, manunuzi na usimamizi wa rasilimali watu." Alisema Mtendaji Mkuu.
Kilahala amesema kuwa kipindi hiki ni muhimu sana kwa mustakabali wa TEMESA hivyo mabadiliko ya utendaji kazi lazima yaendeshwe haraka sana kwa wakati huu ambapo mkakati huo umeanza mara moja hasa katika upande wa utengenezaji wa magari.
Aidha Mtendaji Mkuu amewataka watumishi wa TEMESA kufanya mapinduzi katika utendaji kazi wao ili kutengeneza taasisi itakayokwenda mbele na yenye uwezo wa kuhudumia wateja wake kwa ubora na wakati stahiki.