TEMESA YAFANYA KIKAO CHA WADAU MKOANI TANGA

News Image

Posted On: September 20, 2023

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Tarehe 19 Septemba 2023, umefanya kikao na wadau wanaotumia huduma za Wakala huo Mkoani Tanga ikiwa ni muendelezo wa vikao vya wadau ambavyo Wakala huo umeanza kuvifanya nchi nzima kwa lengo la kusikiliza maoni ushauri na changamoto ambazo wadau wake wanakutana nazo pindi wanapokuwa wanatumia huduma za Wakala huo.

Akizungumza wakati wa kikao kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Regal Naivera, na kuhudhuriwa na wakuu wa Taasisi za Kiserikali zilizoko Mkoani Tanga, wauzaji wa vipuri vya magari pamoja na vilainishi, wamiliki wa karakana teule na binafsi pamoja na maafisa usafirishaji wa Taassisi za Serikali Mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewataka wadau hao wanaotumia huduma za TEMESA, kujitahidi kulipia huduma wanazozipata kwa wakati ili kuiwezesha TEMESA kujiendesha lakini pia akauagiza Wakala huo kuendelea kufanya maboresho ya karakana zake pamoja na huduma wanazotoa ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wadau inaowahudumia.

''Tumeshuhudia maboresho mbalimbali, Mtendaji Mkuu amesema mmeboresha kutokana na msaada mkubwa wa kifedha na uwezeshaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na mama yetu Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, tumesikia habari za mikataba yenu mliosaini baina yenu na na wazabuni wanaosambaza vipuri na vilainishi ili kupunguza muda wa manunuzi na mlolongo mrefu wa upatikanaji wa vipuri, na kwahiyo ni imani yetu kwamba uboreshaji huu unaoendelea utaifanya Taasisi hii kuwa ni Taasisi yenye kuleta tija ilyokusudiwa na Serikali na kupunguza malalamiko ambayo wadau wanalalamika mara kwa mara.'' Amesema Mhe. Kindamba na kuongeza kuwa mikakati na maboresho ambayo yanaendelea yakisimamiwa vizuri kuna uhakika kwamba huduma zinazotolewa na TEMESA zitakuwa ni rafiki.

Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro N. Kilahala, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho kumalizika amesema Wakala umetumia fursa hiyo ya kukutana na wadau wake ili kuwaeleza maboresho ambayo unaendelea kuyatekeleza. ''Tumekuwa tukipokea maoni kutoka kwao, tukajua maeneo gani tuna mapungufu, kuna hatua tumeshaanza kuzichukua basi tunatumia fursa hii pia kuwajulisha kwamba moja mbili tatu tumeshakwishafanya lakini bado mtueleze huduma zetu mnazipokeaje na wapi bado tuzidi kuboresha.'' Amesema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa mikutano hiyo ya wadau ni muendelezo wa kuboresha huduma ambazo Wakala unatoa kwa wadau wake kwasababu ili kumhudumia mtu vizuri lazima usikie maoni kutoka kwake, ujue changamoto anaiona iko wapi na namna gani utajipanga kuboresha zaidi huduma.

Kikao kingine cha Wadau kinatarajiwa kufanyika siku ya Alhamisi Tarehe 21 Septemba Mkoani Pwani ambapo kitahudhuriwa na wadau wanaotumia huduma za Wakala huo Mkoani humo.