WAKURUGENZI WATOA NASAHA KWA WATUMISHI TEMESA DAR ES SALAAM

News Image

Posted On: November 14, 2022

Mkurungezi wa Huduma Saidizi Bi. Josephine Matiro na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Hassan Karonda kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) leo kwa pamoja wamefanya ziara ya kiutendaji kupokea na kusikiliza maoni, changamoto na ushauri kutoka kwa watumishi wa TEMESA Mkoa wa Dar es Salaam. Wakurugenzi hao walianza ziara yao kwa kutembelea kivuko cha Magogoni Kigamboni na kuzungumza na watumishi wa kivuko hicho ambapo moja wapo ya changamoto zilizotolewa na watumishi hao ilikuwa ni changamoto ya vifaa vya kutendea kazi ikiwemo (redio calls),mashine maalumu za kukatia tiketi (POS) kwa ajili ya magari, pikipiki na baiskeli pamoja na vitendea kazi vya kiufundi hasa upande wa mafundi wa kivuko.

Wakijibu hoja hizo kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi na Mkurugenzi wa matengenezo wamewataka watumishi hao kutunza vitendea kazi hivyo na kuweka utaratibu mzuri wa utunzaji wake kwani mara kwa mara watumishi hao wamekuwa wakipatiwa vifaa hivyo. ''Lazima tuwajibike kila mmoja kwa upande wake, kazi yako lazima uipende uitunze na kuiheshimu, Kitu chochote ili kidumu lazima kitunzwe, hivyo ni jukumu lenu kutunza vifaa hivi amesema Matiro na kuwataka kufanya kazi kama timu kwa kutegemeana, kuwa na ushirikiano, upendo umoja na kuheshimiana kila mmoja wao.

Wakiwa katika ofisi za Kikosi cha Umeme zilizopo Keko jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Hassan Karonda ameupongeza uongozi wa Kikosi hicho pamoja na watumishi kwa kuonyesha utendaji mzuri wa kazi katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha. ''Nimepata matumaini makubwa sana na hii taarifa yenu, matokeo yanaonyesha mnafanya vizuri, lakini kuzalisha ni kitu kimoja na kukusanya ni kitu kingine, kama tutazalisha na hatutakusanya hatutakuwa tumefikia malengo yetu, tuongeze jitihada katika kukusanya'' Alisema Mhandisi Karonda na kuwasisitizia kuwa Serikali imewaamini hivyo kila mmoja atimize majukumu yake.

Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bi Josephine Matiro amewaasa watumishi wa Kikosi cha Umeme kutobaguana, kufanya kazi kama ndugu pamoja na kuwa na umoja na mshikamano katika maeneo yao ya kazi.

Ziara ya Wakurugenzi hao ilitamatika katika karakana ya Mt. Depot liyopo Keko jijini Dar es Salaam ambapo walikutana na watumishi wa karakana hiyo ambayo kwa sasa imeunganishwa na karakana ya Vingunguti katika utoaji Huduma. Miongoni mwa maoni waliyotoa watumishi hao ni pamoja na kuomba elimu itolewe kwa mafundi wengi zaidi ili kurahisisha utendaji kazi wao hasa yanapokuja magari ya kisasa pamoja na ombi la wahasibu wa kituo hicho kuomba kupewa mafunzo ya kiuhasibu ili kuweza kufanya kazi zao kwa umakini zaidi.

Mkurugenzi wa Huduma Saizidi, aliwapongeza kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya hasa katika ufuatiliaji wa madeni na ukusanyaji na kuwataka kuanza kujitangaza zaidi ili watu wengi wafahamu kuhusu huduma zao, ''mmefanya kazi nzuri sana, kwa sasa mnatakiwa mjitangaze zaidi ili kazi zenu zionekane huko nje, kuna njia nyingi za kufanya ili watu huko nje wajue kwamba mmefanya mabadiliko'', amesema Matiro na kuwataka kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kazi zao wanazozifanya zinatambulika nje.

Nao Mameneja wa vituo hivyo akiwemo Meneja wa Kikosi cha Umeme Mhandisi Pongeza Semakuwa, Meneja wa karakana ya Mkoa Dar es Salaam Mhandisi Liberatus Bikulamchi pamoja na Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe Kingómbe, kwa nyakati tofauti wamewashukuru viongozi hao kwa kutenga muda wao na kutembelea vituo hivyo kujionea hali halisi ya kiutendaji katika vituo hivyo.