TEMESA KIKOSI CHA UMEME YAWASHA TAA JENGO LA OFISI YA RAISI MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA

News Image

Posted On: February 09, 2024

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA kupitia Kikosi cha Umeme umefanikiwa kusimika mifumo ya Umeme, TEHEMA, Elektroniki, viashiria moto, mifumo ya viyoyozi ya upoozaji hewa (Air Condition) pamoja na lifti katika jengo la Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora linaloendelea kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba mjini Dodoma.

Akizungumza wakati akikagua mifumo ya Umeme iliyosimikwa katika jengo hilo, Meneja wa Kikosi cha Umeme Mhandisi Pongeza Semakuwa amesema jengo hilo limefikia hatua za mwisho kabisa za ujenzi wake huku akiongeza kuwa jengo hilo mpaka sasa ujenzi wake tayari umefikia zaidi ya asilimia 95%.

''Tumejionea taa tulizosimika, tumejionea vitambuzi moto tulivyosimika, mifumo ya viyoyozi, lift iliyosimikwa na TEMESA na haopa nikazie kwamba kwa kipindi kirefu TEMESA ilikuwa haifanyi hizi kazi za lifti na TEHAMA kwa ukubwa wake, lakini kupitia jengo hili tumesimika lifti na mmeiona pale lakini pia tumesimika mfumo mzima wa jengo hili upande wa TEHAMA.'' Amesema Mhandisi Pongeza na kuongeza kuwa Kikosi cha umeme pia kimeweza kuingiza umeme mkubwa kutokea kwenye transfoma kuingia mpaka ndani ya jengo na kwenye jenereta.

''Vitu vyote hivyo tayari vimefanyiwa majaribio na vinafanya kazi vizuri, lakini pia tunategemea kuanza hivi karibuni kazi ya taa za nje za usalama (security lights), ndhani mpaka jengo litakapokuwa limekabidhiwa hiyo kazi itakuwa imekamilika.'' Amesema Mhandisi Pongeza.

Vilevile, Mhandisi Pongeza ameongeza kuwa Wakala uliaminiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya kazi za usanifu za majengo yote ya Serikali yanayojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba na TEMESA imekuwa ikipita mara kwa mara kufanya ukaguzi wa majengo hayo ili kujihakikishai usalama pamoja kutoa ushauri wa kitaaalamu pale inapohitajiwa.

''Hapa sisi tumeshiriki kwenye kusimika hii mifumo, lakini hatujaisimika bila kufuata michoro ambayo imeandaliwa na wataalamu wa ushauri kutoka TEMESA, usimikaji wa mifumo hii yote ikiwemo viyoyozi, njia zake za kupeleka ubaridi ndani pamoja na vile vifaa vya ndani ambavyo vinatoa ubaridi, vyote vimewekwa kwa kufuatisha michoro ambayo imefanywa na wataalamu wetu wa TEMESA upande wa Usanifu. Amesema Mhandisi Pongeza na kusisitiza kuwa TEMESA imefanya kazi hiyo kwa ukamilifu mkubwa huku ukizingatia vigezo na utaalamu.

Kikosi cha Umeme pia kinaendelea na zoezi la kusimika mifumo ya namna hiyo katika jengo jipya la Wizara ya Ujenzi ambalo nalo linaendelea kujengwa katika eneo hilo la Mji wa Serikali huku ujenzi wake ukiwa tayari umefikia zaidi ya Asilimia 50%.

Aidha, kwa upande wa Huduma za Ushauri, Mhandisi Pongeza amesema kuwa Wakala unashiriki katika usanifu na usimamizi wa majengo kadha wa kadha yanayoendelea kujengwa katika mji huo wa Serikali yakiwemo majengo ya Ofisi ya Wizara ya Maji, jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii, Utumishi na Utawala Bora, Jengo la Wizara ya Ujenzi na mengine kadhaa.