TEMESA YAENDELEA NA MAFUNZO YA MFUMO WA MUM KWA LENGO LA KUBORESHA NAMNA BORA YA UTOAJI WA HUDUMA ZAKE

News Image

Posted On: May 05, 2025

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA umeendelea kutoa mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM) kwa wadau wake katika mikoa mbali mbali nchini ukiwa na lengo la kuboresha utoaji wa huduma zake kwa wadau na kuipunguzia Serikali mzigo wa madeni.

Mafunzo haya yamefanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha yakiongozwa na Mhandisi Pongeza Semakuwa, ambaye pia ni Meneja wa Kikosi cha Umeme TEMESA na kuhudhuriwa na maafisa usafirishaji kutoka taasisi za serikali, wamiliki wa gereji teule zilizosajiliwa na TEMESA, pamoja na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali.

Katika mafunzo hayo, Mhandisi Semakuwa amesema kuwa kupitia matumizi ya mfumo wa MUM katika utoaji wa huduma za TEMESA hususan utenngenezaji wa magari ni hatua muhimu katika kuhakikisha uwazi, ufanisi, na ubora wa huduma zinazotolewa kwa taasisi za umma na binafsi.

“Mfumo huu unatoa fursa kubwa ya kuboresha huduma kupitia ufuatiliaji wa kazi kwa wakati halisi, kuweka kumbukumbu sahihi, na kuimarisha uwajibikaji. Mfumo wa MUM umeundwa mahsusi kukidhi mahitaji ya watumiaji”,amesema Mhandisi Semakuwa.

Naye Meneja wa Mkoa wa Arusha Mha. Billy Dionis Munishi amesema kupitia maboresho haya TEMESA imekuwa ikitumia mda mchache kutoa huduma za utengenezaji wa magari na imeongeza idadi kubwa ya utoaji wa huduma zake ikilinganishwa na mwanzo hivyo amewaomba wadau wa TEMESA kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kwa ununuzi wa vifaa vya kisasa na maboresho yanayoendelea hapa nchini.

“Changamoto kubwa iliyokuwa inatukabili ni muda wa kutengeneza magari, maboresho haya yamekwenda kurahisisha utoaji wa huduma hii kwa wakati kupitia pia ununuzi wa vitendea kazi tumekuwa tukitumia muda mchache, lakini pia tumepeleka mafundi kwenye mafunzo ya utengenezaji wa magari yanayoendana na teknolojia ya kisasa” alisisitiza Meneja wa Arusha.

Aidha Washiriki wa mafunzo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata na kusisitiza kuwa mfumo huo utasaidia kubadilisha namna ambavyo matengenezo ya magari ya serikali yamekuwa yakifanyika, kwa kuzingatia uwazi na tija.

TEMESA inaendelea na mafunzo haya nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa mageuzi ya kidijitali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na taasisi za Serikali.