TEMESA INAENDELEA NA UJENZI WA MAEGESHO YA KIVUKO NGOHERANGA
Posted On: January 31, 2025
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa maegesho ya Kivuko eneo la Kikove – Ngoheranga ili kuunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba na Malinyi kupitia vijiji vya Ngalimila na Ngombi ambapo ujenzi ya mradi huo ulianza tarehe 11 Desemba, 2024 na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba, 2025.
Hayo yameelezwa leo tarehe 31 Januari, 2025 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mlimba Godwin Kunambi aliyeulizani lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Gati katika Mto Mnyela kuunganisha Halmashauri ya Mlimba na Malinyi kupitia Vijiji vya Ngalimila na Ngombi.
“Kivuko ambacho kitakwenda kwenye eneo la Kikove - Ngoheranga ni kivuko ambacho kilikuwa kinafanya kazi Kilombero kabla hatutajenga Daraja na Mkandarasi ambaye anakikarabati hiki kivuko ni Songoro na hadi sasa kimefikia asilimia 95 ya kukamilika kwa matengenezo yake”, amesema Eng. Kasekenya.
Aidha Eng. Kasekenya amefafanua kuhusu barabara upande wa Mlimba na Malinyi tayari TARURA kwa kushirikiana na TANROADS wanahakikisha inakarabatiwa ili wananchi wanufaike na huduma ya Kivuko pindi kitakapoanza kufanya kazi.