MTENDAJI MKUU WA TEMESA AWATAKA WATUMISHI KUENDANA NA KASI YA MABADILIKO

News Image

Posted On: October 01, 2025

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala, amewataka watumishi wa wakala huo kuendana na kasi ya mabadiliko yanayoendelea ndani ya taasisi, kwa lengo la kuiboresha zaidi katika utoaji wa huduma bora kwa umma.

Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TEMESA Makao Makuu, Kilahala alisema Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya utendaji kazi kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo mfumo wa TIMIS, ili kuongeza ufanisi na uwazi katika utoaji wa huduma.

“Lazima tuishi kulingana na mabadiliko yanavyoenda. Ubora wa TEMESA sio majengo, ni wana-TEMESA wenyewe. Tunataka TEMESA ya tofauti sana. Tukiyatekeleza haya vizuri, mambo yatakuwa mazuri zaidi,” alisema.

Aidha, amewataka watumishi kujisimamia na kusimamia wenzao kwa kufuata miongozo na kanuni zilizopo ili kuhakikisha taasisi inafikia malengo yake kikamilifu.

Katika hatua nyingine, Kilahala amewasihi watumishi wote kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba, kwa kuwachagua viongozi bora watakaosukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa.

Mtendaji Mkuu aliwahakikishia watumishi kuwa uongozi umechukua kwa uzito maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa, na utaendelea kushirikiana nao kwa karibu katika kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na TEMESA zinakidhi viwango vya ubora vinavyotarajiwa na Serikali pamoja na wananchi.