MTENDAJI MKUU WA TEMESA AWATAKA MAMENEJA KUTAMBUA WAJIBU WAO KIKAMILIFU
Posted On: October 17, 2025
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala, amewataka Mameneja wa TEMESA kutoka mikoa yote nchini kutambua kwa kina nafasi na wajibu wao ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Akizungumza leo Mkoani Morogoro alipokuwa akifungua rasmi kikao kazi cha Mameneja wa Mikoa Wagavi na Wahasibu, Kilahala alisema kuwa meneja ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya TEMESA na hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa weledi, bidii na kuzingatia malengo ya Serikali.
“Naomba tutambue nafasi zetu na umuhimu wetu. Wajibu wetu ni kuhakikisha tunatekeleza dhamira ya Serikali kupitia TEMESA. Tumetumwa kufanya kazi, basi tuifanye kwa ukamilifu wake,” alisisitiza.
Aidha, Kilahala aliwakumbusha Mameneja kuwa wao ni mabalozi wa TEMESA katika maeneo yao ya kazi, hivyo wanapaswa kuwa na uelewa mpana wa majukumu yao na kuhakikisha wanaiwakilisha taasisi hiyo kwa hadhi inayostahili mbele ya wadau wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi, Mhandisi Hassan Karonda, alisema kuwa kikao hicho ni fursa ya kuboresha utendaji wa taasisi kwa kupokea maoni na changamoto kutoka kwa Mameneja, kwa lengo la kuzitafutia majawabu yatakayoongeza ufanisi.