​MTENDAJI MKUU TEMESA AFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA MKOA GEITA

News Image

Posted On: October 19, 2022

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania Lazaro N. Kilahala leo amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Reuben Shigella na kufanya nae mazungumzo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa iliyoko mjini Geita. Katika ziara hiyo ya kiutendaji, Mtendaji Mkuu ameambatana na mwenyeji wake Meneja wa Mkoa wa Geita Mhandisi Mahangaiko Ngoroma, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Hassan Karonda pamoja na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bi. Josephine Matiro.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigella akizungumza na viongozi hao kutoka TEMESA, amewashauri kuimarisha huduma za karakana kiujumla kwakuwa ndizo ambazo zina malalamiko mengi na kuahidi ofisi yake itatoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha TEMESA inatimiza vipaumbele vyake ili iweze kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi mkubwa na aliahidi kulipa deni la shilingi milioni 460 ambazo ni madeni zinadaiwa Taasisi zilizoko chini ya Mkoa huo huku ofisi yake ikidaiwa shilingi milioni 51.

‘’Inaonekana wengi wanaopatiwa huduma na TEMESA hawalipi kwa wakati, tutaita orodha tuone wadaiwa wote sugu na tuhakikishe wanalipa madeni yote hata kidogo kidogo ili TEMESA iweze kujimudu na kuweza kutengeneza magari kwa ufanisi huku ikiangalia namna ya kujikwamua ili ifanye kazi hizi kibiashara’’, alisema Mhe. Shigella.

Aidha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania Lazaro N. Kilahala naye amemueleza Mkuu wa Mkoa changamoto ambazo Wakala umekuwa ukikumbana nazo ikiwemo kuwepo kwa gharama kubwa za vipuri na vilainishi vinavyotumika kufanyia matengenezo kingana kusema kuwa kwa mwaka huu wa fedha TEMESA imejiimarisha kwa kuweka utaratibu ambapo imeorodhesha wazabuni ambao itakuwa inachukua vipuri na vilainishi kutoka kwao bila kupitia kwa watu wa kati ambao ndio waliokuwa wakisababisha gharama kuwa juu.

‘’Mwaka huu tumeweka utaratibu ambapo tumeorodhesha wazabuni tutakaofanya nao kazi pamoja na kuweka rejea ya bei za vipuri husika kwa kila Mkoa, hii itatusaidia kupunguza udanganyifu, vilainishi hapo mwanzo tulikuwa tunaagiza kutoka kwa watu wa kati hali iliyosababisha bei kuwa juu ila kwa sasa tuna mikataba ya moja kwa moja na watengenezaji kwa hiyo bei za vilainishi zimepungua kwa sasa lakini pia muda wa kufanya matengenezo umepungua’’. Amesema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa Wakala pia unaanza kupeleka mafundi wake kwenye mafunzo ili waweze kuendana na mabadiliko na kasi ya Teknolojia za kisasa za magari ambazo zinabadilika siku hadi siku.

Mtendaji Mkuu anaendelea na ziara yake ya kiutendaji hapo kesho ambapo atatembelea Mkoa wa Simiyu.