MTENDAJI MKUU TEMESA AHITIMISHA ZIARA YAKE KIVUKONI MAFIA

News Image

Posted On: November 12, 2022

Lazaro Kilahala, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) pamoja na timu yake, Tarehe 11 Novemba 2022, wamehitimisha ziara yao ya kiutendaji Mkoani Pwani katika kivuko cha MV.KILINDONI kinachotoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati Wilayani Rufiji Mkoani Pwani. Mtendaji Mkuu akizungumza na watumishi wa kivuko hicho amewaagiza kuacha tabia ya kwenda kazini kimazoea na badala yake wafahamu malengo yao yanayotarajiwa kutoka kwa Serikali.

''Sisi kama MV. KILINDONI, huu ni uwekezaji mkubwa wa Serikali umefanyika, yapo matarajio na sisi tuliomo humu maana yake ndio tumepewa dhamana ya kusimamia hayo matarajio, nilisema mwanzoni kazi zetu kubwa sisi ni mbili tu, kutunza chombo hiki lakini pia na kusimamia makusanyo, kwenye makusanyo kuna malengo tunatengeneza kila mwaka, mnakaa wenyewe mnafanya tathmini mnasema bwana kwa mwaka hapa tukikaa sawasawa tutakusanya hiki, halafu baada ya kutambua mtakachokusanya yanakuja matumizi ikiwemo kusaidiana na vituo vingine, kwahiyo tukiona hapa tunayumba kukusanya basi tujue kuna kituo kule kinayumba.'' Alisema Kilahala na kuwataka kuimarisha makusanyo katika kivuko hicho.

Meneja wa Vivuko Kanda ya kati Mhandisi Lukombe Kingómbe, akifunga kikao hicho, ameushukuru uongozi wa Wakala kwa kufika eneo hilo kusikiliza changamoto ambazo watumishi wa kivuko hicho wanapitia na kuahidi timu hiyo itafanya kazi kwa weledi na kwa kujituma kuhakikisha wanakusanya mapato ya kutosha ili kukifanya kivuko hicho kiendeelee na kuahidi atayafanyia kazi maagizo yote ambayo timu hiyo imewapatia, amewataka pia watumishi wenzake kivukoni hapo kupambana na kuhakikisha wanakusanya mapato kwa kadiri ya uwezo wao ili kivuko hicho kiweze kuendelea na kuweza kujiendesha na kutilia mkazo hasa kwenye upande wa mizigo ambayo kwa eneo hilo ndiyo inavushwa kwa asilimia kubwa katika. ''Nataka mtambue kwamba nyie ni watu muhimu sana na sisi kwa umoja wetu tuijtahidi kukusanya mapato kwa nguvu ili tuweze kuuvusha Wakala wetu mbele.'' Alimaliza Mhandisi Kingómbe.