​MTENDAJI MKUU AHITIMISHA ZIARA YAKE KWA KUIPONGEZA KARAKANA YA VINGUNGUTI

News Image

Posted On: December 28, 2021

MTENDAJI MKUU AHITIMISHA ZIARA YAKE KWA KUIPONGEZA KARAKANA YA VINGUNGUTI

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala leo amehitimisha ziara yake ya siku mbili kwa kutembelea karakana za MT. Depot pamoja na karakana ya Vingunguti zilizopo jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na yote, amewapongeza watumishi wa karakana ya Vingunguti kwa kufanya mabadiliko makubwa kwenye karakana hiyo na kuifanya kuwa karakana ya mfano.

Akizungumza na watumishi wa karakana hiyo mara baada ya kumaliza kuikagua mapema leo, Mtendaji Mkuu amesema kazi wanayoifanya karakana ya Vingunguti ndicho ambacho anatamani karakana zote nchini ziige mfano huo.

‘’kuanzia leo hii, tatizo kuhusiana na namna gani tuendeshe Mikoa yetu upande huu wa ufundi nahesabu limeshapata jibu, alisema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa ni wakati sasa TEMESA nzima waige mfano huo huku akimtaka meneja wa karakana hiyo kuendelea kufanya kazi nzuri ili kuufikisha Wakala mahali unapotakiwa kuwa.

''Mnaposema kuwa mnataka kuwa kioo kwa TEMESA nzima, tayari mmeshakuwa kioo, twende tukaibebe hii dhana,tukaubebe huu ukioo tuufikishe na maeneo mengine. Kwa hiyo kwa hilo nyie jukumu lenu ni kuendelea kuyaishi haya, kuendelea kuyatekeleza haya ambayo tumekwisha yaanzisha lakini wakati huo tutamtaka meneja wa hapa (Mhandisi Bikulamchi), namna gani hiki alichoweza kukipanda hapa, tukakipande na maeneo mengine, kwakweli mmenitia moyo sana, mmenipa imani kuwa kumbe hili sio jambo lisilowezekana, hili ni jambo linalowezekana tukishirikiana na TEMESA Dar es Salaam, mmejipanga vizuri na mnastahili pongezi.'' Alimaliza Mtendaji Mkuu.

Mapema asubuhi, Mtendaji Mkuu alianza ziara yake kwa kutembelea na kukagua karakana ya MT. Depot iliyopo Keko jijini Dar es Salaam ambapo pia alipata wasaa wa kuzungumza na watumishi wa karakana hiyo na kuwataka kufanya kazi kwa pamoja ili kuyafikia malengo ya TEMESA.

Mtendaji mkuu amehitimisha ziara yake ya siku mbili jijini Dar es Salaam na anarejea jijini Dodoma kuendelea na shughuli za kujenga taifa.

Tanzania Census 2022