MAFUNDI MAGARI TEMESA WAPIGWA MSASA CHUO CHA TAIFA CHA USAFIRISHAJI TANZANIA (NIT)
Posted On: March 16, 2025
Mafundi thelathini kati ya sitini upande wa matengenezo ya magari kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), leo wameanza rasmi mafunzo ya siku saba ambapo kundi la kwanza la watu thelathini tayari wameanza mafunzo hayo ambayo yanafanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Tanzania (NIT) yakijikita zaidi katika utengenezaji wa mifumo ya Injini na Giaboxi za magari ya kisasa yanayotumiwa na viongozi wa Serikali ambayo yanakuja na teknolojia mpya kila uchwao.
Akizungumza na mafundi hao wakati akifungua mafunzo hayo ya siku saba yanayofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Tanzania (NIT), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde amesema TEMESA kwa sasa inapitia mageuzi makubwa ya utekelezaji wa mkakati wa kuboresha utendaji kazi wake ikiwemo, usimikaji na uboreshaji wa mifumo ya matengenezo ya magari, utaratibu mpya wa malipo kabla (Pre-paid) na uendelezaji wa rasilimali watu ili kufikia viwango vya huduma vinavyotakiwa hivyo ili kuendana na mabadiliko hayo ni lazima mafundi hao pamoja na watumishi wengine wa kada mbalimbali wapigwe msasa ili waweze kuendana na mabadiliko hayo huku akizitaka Taasisi zote za Umma na Wizara zinazohudumiwa na Wakala huo kukubali mabadiliko hayo na kuanza kulipia huduma wanazozipata kutoka TEMESA kabla (Pre-paid) na kwa wakati ili kuuwezesha Wakala huo kujiendesha.
‘’Serikali imeamua kuifanyia TEMESA maboresho makubwa ili iweze kuihudumia Serikali kwa ufanisi na tija hivyo ninawaomba wale wote mnnaohudumiwa na TEMESA muunge mkono mabadiliko haya ili azma hii muhimu kwa mustakabali wa Taifa iweze kutimia.’’ Amesema Dkt Msonde na kuongeza kuwa mabadiliko hayo ni muhimu kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.
Naibu Katibu Mkuu pia ameziomba Taasisi zote za Umma na Wizara zote kuhakikisha zinaingia kwenye mfumo mpya wa kidigitali wa matengenezo ya magari unaojulikana kama MUM ili magari yote ya Serikali yaweze kuandikishwa humo na kujulikana.
‘’Tunataka gari lolote la Serikali linapokuja kwenye karakana zetu kutengenezwa ni lazima liingizwe kwenye mifumo ya MUM, tuwe tunajua wakati wote hata sisi tukiwa Wizarani tujue gari fulani la Serikali linatengenezwa Mkoa wa Katavi liko kwenye hatua fulani.’’ Amesema Dkt. Msonde na kuongeza kuwa, katika mifumo hii ya kutengeneza mikakati ya kuboresha TEMESA wamebadilisha mfumo na kuleta mfumo wa ulipaji wa kabla ya matengenezo (Pre-paid).
‘’Ninafahamu huko nyuma tulikuwa na mfumo tunaoutumia ambao umetufikisha wakati mwingine hapa tulipo. Serikali imeamua sasa kuwa na mfumo wa kulipa mapema kabla ya huduma au mara tu huduma inapokamilika ili kuepuka kutengeneza madeni kama ilivyokuwa hapo awali.’’ Aliongeza Naibu Katibu Mkuu.
Dkt. Msonde pia amewataka mafundi hao wanaopatiwa mafunzo kuhakikisha wanajifunza kwa bidii na kutumia ujuzi wanaopatiwa kwenda kufanya mapinduzi makubwa katika karakana zao wanaporudi katika ubora wa hali ya juu ili kusiwepo tena na malalamiko ya matengenezo hafifu katika karakana za TEMESA.
‘’Mnaporudi vituoni tumieni ujuzi huu mliopata kuwafundisha na wenzenu maana wanasema ukitaka kukimbia haraka kimbia mwenyewe lakini ukitaka kufika mbali kimbia na wenzio, TEMESA tunataka kufika mbali.’’ Alisisitiza Dkt. Msonde.
Awali, akisoma taarifa fupi kwa mgeni rasmi, Mtendaji Mkuu TEMESA Lazaro Kilahala amesema TEMESA inao jumla ya mafundi mia tatu na sitini na moja na imeanza kuwapa mafunzo mafundi hao kwa uchache na itahakikisha inawapatia mafunzo mafundi wote ili wawe na ujuzi unaolingana, Kilahala amesema mafundi thelathini kati ya sitini wanaaanza mafunzo yao katika Chuo hicho na baada ya siku saba watafuatiwa na kundi lingine la mafundi thelathini ili kuhitimisha mafunzo hayo.
Kilahala ameongeza kuwa mafunzo haya ni maalum sababu yanajielekeza zaidi katika kujifunza kwa vitendo (practical training) ili mafundi hao watoke wakiwa tayari kwenda kuhudumia magari ya Serikali kwa kujiamini. Amesema Mafunzo hayo yatajikita katika utengenezaji wa mifumo ya Injini na Giaboxi za magari ya kisasa yanayotumiwa na viongozi. Katika awamu hii ya kwanza jumla ya mafundi sitini ambao wamejumuisha jumla ya mafundi wawili toka kila mkoa/kituo watapatiwa mafunzo haya. Mafunzo haya yatakuwa endelevu na yatawafikia mafundi wote wa TEMESA.
“Tumeanza safari ya mabadiliko ila tumeona tukianza na wewe ndio tutafika, itendee haki nafasi unayoipata ya mafunzo, haya ni mafunzo muhimu sana ambayo yanakwenda kubadili mustakabali wa Taasisi yetu.” Alisema Kilahala na kuongeza kuwa TEMESA imeamua kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuwapatia Mafundi Magari wake mafunzo maalum yanayojielekeza kuwezesha mafundi hawa kutengeneza magari ya kisasa kwa ustadi na kujiamini huku ikiendelea na jitihada za kupata fursa zaidi za mafunzo kupitia vyuo vingine hapa nchini pamoja na mawakala wa watengenezaji wa magari hapa nchini kama vile Toyota na Nissan ili kuhakikisha mafundi wa TEMESA wanapata ujuzi unaoendana na mabadiliko ya Teknolojia ya magari.
Aidha, Kilahala ameongeza kuwa kupitia mafunzo haya TEMESA inakusudia kuondoa changamoto ya kuwa na mafundi wenye ujuzi mdogo au wasiojiamini hivyo kuongeza ufanisi katika matengenezo ya magari ya Serikali huku akisema kuwa wanaendelea kutafuta mafundi kutoka maeneo mbalimbali wenye ujuzi ili kuoboresha kada hiyo ya ufundi wa magari.
‘’Sambamba na kutoa mafunzo kwa mafundi tulionao, Wakala pia unaendelea na jitihada za kutafuta mafundi wenye ujuzi na uzoefu mkubwa, wabobevu popote walipo ndani ya Tanzania ili kuimarisha zaidi uwezo wetu wa kuhudumia magari ya Serikali kwa ufanisi na tija ya hali ya juu.’’Alimaliza Mtendaji Mkuu.
TEMESA kwa sasa inapitia mageuzi makubwa ya utekelezaji wa Mkakati wa Kuboresha Utendaji kazi wake ikiwemo; usimikaji na uboreshaji wa mifumo ya Matengenezo ya magari, utaratibu mpya wa malipo wa Pre-paid, na uendelezaji wa Rasilimali watu ili kufikia viwango vya huduma vinavyotakiwa.