NAIBU KATIBU MKUU UJENZI ARIDHISHWA NA MABORESHO YA TEMESA

News Image

Posted On: August 05, 2026

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, ameupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa maboresho makubwa ya utoaji wa huduma, hususani matumizi ya teknolojia yanayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Dkt. Msonde amesema hayo leo, Agosti 5, 2026, alipotembelea banda la TEMESA katika Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Kilimo (NaneNane 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni, jijini Dodoma.

Dkt.Msonde Amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na TEMESA, akieleza kuwa uimarishaji wa huduma za kidijitali pamoja na ongezeko la ubora wa mafundi umeongeza ufanisi wa wakala huo.

“Kilichonifurahisha zaidi ni uimarishaji wa mafundi. Sasa wanafanya kazi kwa weledi mkubwa na wanatengeneza magari kwa ubora. Kwa kweli TEMESA mmenifurahisha sana,hongereni sana” amesema Dkt. Msonde.

Aidha, amesema Serikali na wananchi wanaiamini TEMESA kutokana na mchango wake katika kulinda usalama wa magari ya Serikali na kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za umma. Amewataka viongozi na watumishi wa wakala huo kuendelea kubuni na kuboresha huduma kwa kutumia teknolojia.

Kwa upande wake, Meneja Masoko na Uhusiano kwa Umma TEMESA, Bi. Martha Joachim, amesema miongoni mwa maboresho yaliyofanywa ni kuhuisha huduma ya ukodishaji wa mitambo kupitia Mfumo wa TIMIS, ambapo wateja sasa wanaweza kuwasilisha maombi ya ukodishaji kwa njia ya kidijitali, hatua iliyopunguza urasimu na muda wa kupata huduma.

Maonesho hayo yenye kauli mbiu “Tambua Soko, Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050”, yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 8 Agosti, 2026.