TEMESA YAENDELEA KUCHOCHEA TIJA NA UBUNIFU KUPITIA MAONESHO YA NANENANE 2026
Posted On: August 04, 2026
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) unashiriki katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo – NaneNane 2026, yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, yaliyozinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Maonesho hayo yanayofanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026, yamebeba kaulimbiu isemayo “Tambua Soko; Ongeza Tija; Tekeleza Dira 2050,” ikiwa ni wito kwa wadau mbalimbali kutumia fursa, maarifa, teknolojia na ubunifu kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya Taifa. Kupitia ushiriki wake, TEMESA inatoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu huduma mbalimbali za kihandisi zinazotolewa na Wakala, ikiwemo matengenezo ya magari na mitambo, huduma za umeme na mifumo ya majokofu, vipando na viyoyozi, ushauri wa kihandisi, Ukodishaji wa mitambo pamoja na huduma za vivuko.
Aidha, maonesho haya yanatoa fursa kwa TEMESA kuendelea kuelimisha, kushirikiana na kujenga uhusiano na wadau kutoka sekta mbalimbali, hususani katika matumizi ya teknolojia na huduma za kihandisi zinazochangia kuongeza ufanisi, tija na thamani katika shughuli za uzalishaji. TEMESA inawaalika wananchi wote wanaotembelea Maonesho ya NaneNane 2026 kufika katika banda la Wakala lilioko katika banda kubwa linaloitwa ''Government Pavillion 1 banda nambari 2 kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na fursa mbalimbali za kushirikiana na TEMESA.