MABORESHO KARAKANA TEMESA ARUSHA KUCHOCHEA KASI YA HUDUMA BORA

News Image

Posted On: August 28, 2024

Meneja wa TEMESA Mkoa wa Arusha Mha. Elirehema Mmari, ameishukuru Serikali kwa kuuwezesha Wakala kuendelea kufanya maboresho makubwa ya karakana Tanzania nzima kwa kununua vifaa vya kisasa na kuanza ujenzi wa karakana za kisasa.

Akizungumza leo Agosti 28 ofisini kwake, Mhandisi Mmari amesema maboresho makubwa yanayofanyika yanaleta muamko mpya kwa utoaji huduma wa TEMESA.

Mhandisi Mmari amesema maboresho hayo yanahusisha ujenzi wa karakana, ununuzi wa vifaa vya kisasa, ujenzi wa ofisi na maeneo ya kukagulia na kufanyia ukarabati wa magari ambapo ukarabati huo utakapokamilika utachochea kasi na ubora wa utolewaji wa huduma kwa wadau wake.

“Ukarabati huu utakapokamilika utaleta manufaa mkubwa sana kwetu sisi watumishi wa Arusha, wananchi wa Arusha Pamoja na watanzania kwa ujumla kwasababu tutakuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi,” amesema Mhandisi Mmari.

“Ukishakuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi unakuwa na uhakika na hata kazi utakazokuwa unazifanya zinakuwa na ubora na ni matumaini yetu kwamba wateja wetu watakuwa wamepata huduma ambayo serikali imeitegemea”, Alisisitiza.

Mhandisi Mmari amesema serikali kupitia TEMESA imenunua vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi kuendana na mabadiliko ya teknolojia na uundwaji wa magari ya kisasa, ambapo ina vifaa vya kisasa vya kukagulia magari na kubaini tatizo na namna ya kulitatua kwa muda mfupi.

Aidha Mhandisi Mmari amewaomba wadau wa nje na ndani ya mkoa wa Arusha kutembelea karakana hiyo, ili iweze kujionea maboresho mbalimbali yaliyofanyika na kupatiwa huduma bora na stahiki.