WAJUMBE BODI YA USHAURI TEMESA WAPONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MIRADI

News Image

Posted On: October 02, 2020

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA MAB) wameupongeza Wakala huo kwa kufanya juhudi kubwa kuhakikisha miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 inatekelezwa na kumalizika kwa wakati.

Wajumbe hao wametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki hii wakati walipofanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na TEMESA ikiwemo ukarabati wa karakana za mikoa mbalimbali, ujenzi wa karakana mpya katika vituo, ukarabati wa vivuko, ujenzi wa maegesho ya vivuko na mabanda ya kupumzikia abiria pamoja na ujenzi wa vivuko vipya. Wakiwa katika ziara hiyo, wajumbe hao walianza kwa kutembelea karakana ya mkoa wa Singida ambapo Meneja wa mkoa huo Mhandisi Awadh Suluo alipata wasaa wa kuwapitisha kujionea ujenzi wa majengo mapya ya karakana hiyo ukiwa tayari umekamilika ambapo kwa mujibu wa meneja, muda wowote kuanzia sasa watumishi watahamia kwenye majengo hayo mapya.

Ziara ya wajumbe hao iliendelea kwa kutembelea mkoa wa Simiyu ambapo walipokelewa na meneja wa TEMESA mkoa huo Mhandisi Ramadhani Ally pamoja na menejimenti yake ambapo walianza kwa kukagua karakana ya mkoa huo ambayo ipo kwenye eneo la kukodi na baadae wakapata wasaa wa kutembelea eneo la ujenzi wa karakana mpya ya kisasa ambayo inajengwa katika eneo la Nyaumata ambapo ofisi za serikali mbalimbali zinajengwa maeneo hayo huku mji huo ukitazamiwa kua mji wa serikali hapo baadae baada ya maofisi yote ya serikali kukamilika. Ujenzi wa ofisi hizo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kwa mujibu wa mkandarasi Vikosi vya Ujenzi.

Wajumbe wa bodi hiyo walimalizia ziara yao mkoani Mwanza ambapo walipokelewa na meneja wa mkoa huo Mhandisi Hassan Karonda. Walianza kwa kukagua utendaji kazi katika kivuko cha Kigongo Busisi ambapo Mhandisi Karonda aliwaelezea jinsi utendaji kazi wa vivuko hivyo unavyoendelea na walipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na kituo hiko katika kuhakikisha shughuli za uvushaji wa abiria na mali zao zinaendelea katika ubora unaotakiwa.

Halikadhalika wajumbe hao walipata wasaa wa kukagua karakana ya mkoa huo ambayo inafanyiwa ukarabati mkubwa wa majengo yake ambayo mengi yalikuwa machakavu, waliweza kujionea jinsi ujenzi huo unavyoenda kwa kasi na walimuagiza mkandarasi, Vikosi vya Ujenzi kuhakikisha anakimbizana na muda na kumaliza ujenzi huo mapema kama mkataba unavyomtaka.

Baadae wajumbe hao walitembelea yadi ya Songoro iliyopo Ilemela kujionea ujenzi unaoendelea wa vivuko viwili vipya vya Ukara Bugorola Pamoja na Chato Nkome ambapo mkandarasi anayesimamia ujenzi wa vivuko hivyo Major Songoro aliwahakikishia kwamba vivuko vyote ujenzi wake unaendelea vizuri na umefikia takribani asilimia tisini na vitakamilika hivi karibuni kwani vifaa vyote vilivyokuwa vinasubiriwa vimekwisha wasili na vitaanza kufungwa haraka iwezekanavyo.

Awali wajumbe hao walikagua maendeleo ya ukarabati wa kivuko cha MV.Sengerema ambao unaendelea na kwa mujibu wa Major Songoro, ukarabati huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Novemba.

Ziara ya wajumbe hao ilimalizika kwa kutembelea kivuko kipya cha MV.Ilemela kinachotoa huduma kati ya Kayenze, visiwa vya Bezi na Ukerewe ambapo pia walipata wasaa wa kukagua mabanda ya kupumzikia abiria yaliyojengwa katika kituo hicho ambapo upande wa Bezi ujenzi bado unaendelea.