MILIONI 400 ZANG'ARISHA BARABARA USHETU
Posted On: September 08, 2021
Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA kupitia Kikosi chake cha Umeme (Corporation Sole) umesimika taa za kumulika mitaa barabarani (street lights) zipatazo 100 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, takribani kilometa 52 kutoka Wilayani Kahama mjini Shinyanga. Taa hizo zilizogharimu takribani shilingi milioni 400 za Kitanzania zimesimikwa katika barabara ya kuelekea Wilaya ya Kahama katika Kijiji cha Mitonga kitongoji cha Mitonga A na Nyamilangano na zimekava eneo la kilometa takribani tatu.
Akizungumza na waandishi wa Shirika la Utangazaji nchini TBC wakati wa kukagua taa hizo, Meneja wa Kikosi cha Umeme Mhandisi Pongeza Semakuwa amesema kuwa mradi wa usimikaji wa taa hizo ulikuwa wa muda wa miezi sita na kikosi hicho kimeukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa gaharama nafuu kutokana na kuzalisha nguzo hizo wenyewe na hiyo imesababisha kupungua kwa gharama zake kwani kuagiza nguzo moja ya taa hizo kutoka nje ya nchi kungegharimu zaidi ya shilingi milioni tatu na nusu wakati kikosi chake kimetumia shilingi million mbili kwa kila taa moja na hivyo kuokoa zaidi ya shilingi milioni moja na nusu.
‘’Nguzo hizi mnazoziona zimezalishwa kwenye karakana yetu iliyopo Dar es Salaam na tumekuwa tukifanya kazi hiyo kwa muda mrefu na hali hiyo imepelekea hata gharama za usimikaji wa taa hizi kupungua kutokana na kutengeneza wenyewe malighafi hizi’’. Alisema Mhandisi Pongeza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa maeneo hayo wametoa shukrani zao za dhati kwa Serikali kwa kuweza kuwapelekea mradi huo kwani umesaidia kuwaondolea adha kubwa waliyokuwa nayo hapo awali ikiwemo kuvamiwa na fisi wawapo barabarani nyakazi za usiku, lakini pia uhalifu ukiwa umepungua kutokana na uwepo wa taa hizo pamoja na kupungua kwa ajali ambazo zilikuwa zikisababishwa na uwepo wa giza totoro katika barabara hiyo na kusababisha kutoonekana vizuri hasa kwa watumiaji wa vyombo vya moto na baiskeli wanaoishi katika vijiji hivyo.
Mkazi mmoja wa kijiji cha Matiza Mitonga, aliyejitambulisha kwa jina moja la Magolanga, amesema taa hizo zimewapa uhuru wa kutembea usiku bila uwoga tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo walikuwa wakitembea eneo hilo kwa uwoga kutokana na giza na pia ameishukuru Serikali kwa mradi huo na kuiomba kuendelea kuwatekelezea miradi mingine itakayowanufaisha zaidi.
Nao wafanyabiashara walioko kando ya barabara hiyo hawakuwa nyuma, Flora Leonidas, mfanyabiashara anayeuza chakula maarufu mamantilie, ameishukuru Serikali kwa kuwasimikia taa hizo na kusema kuwa taa hizo zinawasababishia kufanya biashara zao kwa uhuru na wanaweza kufanya biashara zao mpaka saa sita za usiku kukiwa na mwanga wa kutosha tofauti na hapo awali ambapo iliwabidi wafunge biashara zao mapema saa mbili kwa kuhofia giza.
Pendo Samweli, mkazi wa Nyamilangano ambao nao mradi huo wa taa za barabarani umepita kando ya eneo analofanyia biashara zake za kuuza chakula, amesema taa hizo zimewaletea faida kubwa kwani hapo awali iliwabidi kuwa wanakodisha taa kwa ajili ya kufanyia biashara usiku lakini kwa sasa hawakodishi tena taa hizo na badala yake mwanga wa taa zilizofungwa na Serikali unawamulikia biashara zao na hivyo wameweza kutunza fedha yao ambayo awali waliitumia kulipia huduma ya taa za kukodi.
Simoni Makonda, dereva wa pikipiki maarufu bodaboda naye ameishukuru Serikali kwa kusimikiwa taa hizo katika barabara hiyo na kusema kuwa zimesababisha kupungua kwa ajali kwa kuwepo mwanga wa kutosha, wameweza kufanya kazi mpaka usiku mwingi na pia kipato chao kimeongezeka kwasababu ya kufanya kazi hiyo mpaka usiku wa manane kutokana na kuwepo kwa mwanga wa kutosha.
Mhandisi Pongeza ametoa rai kwa taasisi za Serikali na za binafsi ambazo zinahitaji huduma kama hiyo kuitumia TEMESA kwani wako tayari kufanya kazi hiyo sehemu yoyote ile ya nchi kwa gharama nafuu.
Mhandisi pia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kukiamini Kikosi cha Umeme na kuendelea kukipa miradi mbalimbali ya taa za barabarani kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na amewasishi wakazi wa maeneo hayo kuutunza mradi huo ambao amesema unatarajia kudumu kwa muda wa zaidi ya miaka kumi bila kuwa na tatizo lolote.
MWISHO