WADAU WAOMBWA KULIPA PESA KWA WAKATI KUCHOCHEA HUDUMA BORA KUTOKA TEMESA
Posted On: March 26, 2024
Wadau wanaotumia huduma za TEMESA Mkoa wa Iiringa wameombwa kuulipa Wakala huo madeni yake kwa wakati ili iweze kujiendesha vyema na kuzidi kuboresha huduma zake.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala huo Bi Josephine Matiro Tarehe 20 Machi, 2024 alipokuwa akizungumza na wadau wanaotumia huduma za Wakala huo kwenye kikao cha wadau kilichofanyika katika ukumbi wa Royal Palm ulioko mkoani Iringa na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Kheri James.
Matiro amesema TEMESA ni taasisi ambayo inajiendesha yenyewe kwa kufanya kazi lakini kumekuwa na changamoto ya wateja wake kutokulipa madeni kwa haraka pindi wapatapo huduma ambapo hali hii inapelekeaTEMESA kutokufikia malengo yake.
“TEMESA sisi ni taasisi ambayo inajiendesha yenyewe, tunafanya kazi, tunachokizalisha tunatumia kujiendesha, lakini tatizo kubwa ni kwamba tunafanya kazi lakini hatulipwi madeni kwa wakati”alisisitiza.
Aidha Bi Matiro amesema kupitia vikao hivi TEMESA inapata wasaa wa kuzungumza na wateja wake, kujadili mambo mbalimbali yahusuyo huduma zitolewazo na kuwahimiza wadau walipe madeni yao kwa wakati ili Taaasisi iweze kuendelea vizuri.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Kheri James ameipongeza TEMESA kwa mafanikio makubwa ya kuleta huduma ya utengenezaji wa magari kwa njia ya karakana inayotembea (mobile workshop) ambapo mteja mwenye magari mengi hatopata usumbufu wa kuyapeleka magari yote kwa ajili ya matengenezo bali atafwatwa mahali alipo.