SPIKA TULIA AIPA KONGOLE TEMESA
Posted On: June 07, 2024
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson ametoa pongezi kwa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa kuendelea kufanya maboresho katika utoaji wa huduma zake upande wa karakana ambapo moja ya maboresho makubwa aliyoyashuhudia ni uanzishwaji wa karakana inayotembea ambayo inatoa huduma mahala popote kwa ajili ya magari yaliyopata hitilafu maeneo yaliyo mbali na karakana za Mikoa na Wilaya pamoja na kuyafata magari mahali yaliko kwa ajili ya kutoa huduma ya matengenezo kinga (Service).
Dkt. Tulia ametoa pongezi hizo Tarehe 27 Mei, 2024 wakati alipotembelea Banda la Wakala huo katika Maonesho ya Sekta ya Ujenzi kuelekea Bajeti ya Wizara hiyo yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma ambayo yanashirikisha Taasisi zote zilizoko chini ya Wizara ya Ujenzi. Spika wa Bunge, aliambatana na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mha. Balozi Aisha Amour kukagua mabanda mbalimbali ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.
Dkt. Tulia amesema kuwa, kwa ukubwa wa Nchi yetu, ni muhimu sana kuwa na magari mengi ya namna hiyo ambayo yanarahisisha utoaji wa huduma na kuokoa muda huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kutoa fedha za kufanikisha maboresho hayo lakini pia kuwezesha uwekezaji huo kutimia.
‘’Niwapongeze TEMESA kwa kuanzisha huduma ambayo mnaweza kumfuata mteja alipo badala ya yeye kuja kuleta gari, wakati mwingine gari inakuwa imeharibika mahali ambapo haliwezi kutembea na badala yeye atafute gari nyingine ya kuivuta, sasa anaweza nyinyi TEMESA mkamfuata alipo na mkatengeneza muda wowote saa 24, ninawapongeza sana kwa hatua hizo’’ Amesema Dkt. Tulia.
Dkt. Tulia ameongeza kuwa anaamini kwa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kuendelea kusikiliza ushauri ambao Bunge lake linatoa wakati wote, magari hayo yataendelea kuongezeka ili angalau kila mahali kuwepo na magari ya aina hiyo kwasababu pamoja na kuwa ni huduma, lakini pia ni biashara.
‘’Nawataka na nyinyi muwe mmesonga zaidi kuliko wengine ili muipatie Serikali mapato kupitia utengenezaji wa magari’’, amesema Dkt. Tulia huku akiongeza kuwa yale yaliyokuwa yanazungumzwa huko nyuma kuhusu utoji huduma za TEMESA yanaendelea kufanyiwa kazi.
‘’Kwakweli tunatarajia mabadiliko makubwa kama ambavyo kuna mabadiliko kwenye Sekta hii ya Ujenzi, basi tunawatarajia na ninyi huduma zenu zibadilike kulinganana haya mabadiliko makubwa yanayofanyika’’. Alisema Spika huyo wa Bunge.
Maonesho ya Sekta ya Ujenzi yalishirikisha Taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo ikiwemo Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS), Wakala wa Majengo Nchini (TBA), Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Chuo cha Ujenzi Morogoro (ICOT), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) pamoja na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (EQRB).