WANANCHI WA KANDA YA KUSINI WAENDELEA KUMIMINIKA KATIKA BANDA LA TEMESA NANENANE NGONGO
Posted On: August 05, 2025
Wananchi kutoka mikoa ya kusini mwa Tanzania wameendelea kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.
TEMESA kupitia banda lake imejipambanua kwa kutoa huduma mbalimbali kwa wadau wake, ikiwemo huduma ya ukaguzi wa magari bure kwa kutumia vifaa vya kisasa vya kuchunguza ubora wa mifumo ya magari. Huduma hiyo imekuwa kivutio kikubwa kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi kwa ujumla waliotembelea maonesho hayo, huku wakipata elimu ya namna bora ya kutunza na kuhudumia vyombo vya usafiri.
Mbali na ukaguzi wa magari, TEMESA pia inatoa elimu kuhusu huduma zake nyingine kama vile matengenezo ya magari ya Serikali, usimikaji wa mfumo wa umeme, huduma za vivuko pamoja na matumizi ya mfumo wa kidijitali wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM).
TEMESA Lindi inawakaribisha wananchi wote kuendelea kutembelea banda lao katika viwanja vya Ngongo, kujifunza, kufaidika na huduma zinazotolewa, na kwa pamoja kuunga mkono jitihada za maendeleo katika sekta ya usafiri, kilimo, mifugo na uvuvi.