KATIBU TAWALA SINGIDA AWATAKA TEMESA KUJIENDESHA KIBIASHARA
Posted On: March 31, 2023
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt.Fatma Mganga amewataka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) mkoani hapa kujiendesha kibiashara ili kuipunguzia mzigo Serikali ambayo imekuwa ikitoa fedha nyingi kuendesha taasisi hiyo. Mganga ambaye alikuwa mgeni rasmi ametoa ombi hilo leo Machi 29, 2023 wakati akifungua kikao cha wadau wanaotumia huduma za karakana ya TEMESA Mkoa wa Singida ambacho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Makao Makuu Dodoma, Mhandisi Hassan Koronda.
“Tengenezeni magari kwa ubora na weledi punguzeti gharama za uendeshaji ili muisaidie Serikali na mkimbiliwe na wateja” alisema Dkt. Mganga.
Aidha,Dkt. Mganga aliwataka TEMESA kutumia fursa waliyonayo kutoka nje kujitangaza ili wafahamike badala ya kukaa tu ofisini na akaishauri kuanza kutumia TEHAMA kwa ajili ya kupata mrejesho kutoka kwa wateja wao ikiwemo kupitia ujumbe mfupi.
Dkt. Mganga alihimiza TEMESA kutoa mafunzo kwa madereva ya uendeshaji wa magari ili wajue mbinu ya kuyatunza ukizingatia kuwa ni wadau wao na akaomba waanzishe
kitengo cha uoshaji wa magari ili iwe motisha kwa wateja wanaowapelekea vyombo vyao vya moto.
Akizungumzia madeni yanayodaiwa na TEMESA aliomba apewe orodha ya wadaiwa wote zikiwepo Taasisi za Serikali ili aweze kuonana na wahusika waanze kulipa madeni hayo kwa awamu.
“Serikali inayo matarajio makubwa kuona mnafanya kazi zenu kwa kuzingatia misingi ya sheria za utumishi wa umma na kanuni zake kwa kutumia Taaluma zenu kutunza mali za umma hasa magari na miundombinu ya umeme kwani nagharimu fedha nyingi,” alisema Dkt. Mganga.
Aidha, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA , Mhandisi Hassan Koronda alisema Serikali imekua ikitenga fedha kila mwaka na mwaka huu wa fedha, kiasi cha Shilingi Bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa karakana kumi na mbili katika mikoa mbalimbali ukiwemo Mkoa wa Singida ambao ujenzi wake wa awamu ya kwanza tayari umekamilika.
Aidha, Mhandisi Koronda alisema Serikali imetoa kiasi cha fedha Sh.509.8 Milioni kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa kwa upande wa umeme, TEHAMA na mitambo kwa karakana za mikoa yote Tanzania kwa lengo la uboreshaji utendaji wa kazi.
Mkuu wa Magari, TEMESA Mkoa wa Singida, Erasto Cheza akitoa taarifa ya mikakati ya utendaji wa kazi alisema wameyaondoa malalamiko yaliyokuwepo awali kwa kuyatambua na kuandaa mikakati ya kuyamaliza kabisa kwa kushirikiana na wadau wao, mabadiliko ya tabia, matendo na mwenendo kwa kupata elimu ya kuendana na mahitaji ya wateja. Cheza alitaja majukumu yao makubwa kuwa ni kufanya matengenezo ya Magari, pikipiki na Mitambo ya Serikali, kufanya matengenezo na Usimikaji wa Mifumo ya Umeme, Mabarafu, viyoyozi na Elektroniki, kufanya matengenezo ya taa za kuongozea magari na taa za barabarani (Street Lights), kutoa ushauri wa Kitaalamu katika nyanja za uhandisi wa Ufundi, Umeme na Elektroniki,kushauri usimikaji wa mifumo mipya ya uhandisi wa Ufundi, Umeme na Elektroniki na kufanya usanifu na usimamizi wa usimikaji wa mifumo ya uhandisi wa Ufundi.