SERIKALI YATOA BILIONI 66.5 KUTEKELEZA MIRADI TEMESA

News Image

Posted On: September 25, 2019

Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Katibu Mkuu na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kupitia Mtendaji Mkuu wamesaini mkataba wa utendaji kazi wa Wakala huo ambapo ndani yake ipo miradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 66.5 itakayotekelezwa na TEMESA katika mwaka huu wa fedha 2019/2020.

Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Mhandisi Isack Kamwelwe alipokuwa akizungumza wakati akizindua rasmi bodi ya Ushauri ya Wakala huo jijini Dar es Salaam itakayoongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Mhandisi Idriss Mshoro. Mhandisi Kamwelwe amesema kati ya fedha hizo, Wizara imetoa kiasi cha shilingi bilioni 22.6 ili kusaidia mchakato huo.

‘’Hivi karibuni mtaona jinsi serikali ilivyochukua hatua na juhudi za makusudi kuiboresha TEMESA kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Huduma za Ufundi kutoka shilingi bilioni 17.5 hadi kufikia shilingi bilioni 53.1 ni jukumu la bodi kuhakikisha inasimamia kwa karibu matumizi ya fedha hizo baada ya serikali kufanya juhudi zote.’’ Alisema Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe Aliongeza kuwa Wizara mpaka hivi sasa tayari imekwishatoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 12.5 kwa ajili ya kutekeleza maboresho hayo.

Kuhusu madeni ambayo TEMESA inazidai Taasisi za Umma na Wizara, Mhandisi Kamwelwe alisema Wizara imekwishawasilisha barua Wizara ya Fedha na Mipango ya kuomba deni la shilingi bilioni 19.7 lilipwe mara moja na Hazina ambapo alisisitiza hatua hiyo itasaidia siyo tu kujiimarisha bali pia kulipa madeni ya Wazabuni wanaoidai.

Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Mhandisi Japhet Maselle, akifungua kikao hicho alimshukuru Waziri Kamwelwe kwa kuteua bodi hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano wa karibu ili kufanikisha malengo.

‘’Naomba nikushukuru kwa uteuzi wa Bodi ya Wakala na uamuzi wako wa kuizindua leo ili iweze kuanza kazi rasmi, aidha nikuombe utakapokuwa umemaliza uzinduzi wa bodi, uwakabidhi wajumbe wa bodi nyaraka muhimu za kufanyia kazi ambazo zimeandaliwa na Wakala kufuatia maelekezo yako katika barua yako wakati wa uteuzi wao,’’ aliongeza Mhandisi Maselle.

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Mhandisi Idriss Mshoro alimshukuru Waziri Kamwelwe kwa kuwaamini yeye na wajumbe wenzake kuitumikia bodi ya Wakala huo ambapo aliongeza ni jukumu kubwa wamepewa na kuahidi kutimiza majukumu hayo na matarajio ya serikali na wizara kwa ujumla.

Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) inaundwa na wajumbe Cunbert Kapilima kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Boniface Kulaya kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Dkt Benjamin Ndimila kutoka Chuo cha Usafirishaji (NIT), Mhandisi Deogratias Nyanda kutoka Shirika la Nyumbu (TACT) pamoja na Sunday Hyera kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Bodi hiyo imeanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake.