Serikali yataka uzalendo, pamoja na huduma bora vivukoni

News Image

Posted On: December 04, 2017

Baadhi ya Watumishi wa Kivuko cha Kigongo Busisi Mwanza wakiwa na Bi. Aveline Mbunda (wa pili Kulia) Afisa Masoko kutoka TEMESA Makao Makuu

Baadhi ya Watumishi wa Kivuko cha MV. TEMESA Mwanza wakiwa na Bi. Aveline Mbunda (wa kwanza kushoto) Afisa Masoko kutoka TEMESA Makao Makuu

Mkuu wa Kivuko cha Kigongo-Busisi Mwanza Bwana Kashindi Hussein (aliyesimama) akimkaribisha Bi. Aveline Mbunda (aliyeketi kulia kwake) kuongea na watumishi wa kivuko cha Kigongo-Busisi Mwanza


SERIKALI imewataka watumishi wa umma wanaofanya kazi kwenye vivuko nchini kutanguliza uzalendo, uadilifu na kutumia lugha ya unyenyekevu kuwakaribisha abiria ili vivuko vya Serikali viweze kuwa kimbilio la wananchi kutokana na kuboreka kwa huduma kwa mteja.

Agizo hilo lilitolewa jana na Afisa Masoko wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kutoka makao makuu , Bi Aveline Mbunda wakati wa semina kwa watumishi wa Kivuko cha Luchelele-Ilunda ambapo alisema huduma zitolewazo na Serikali ni bora na salama kwa abiria.

Bi. Mbunda alisema kuwa Serikali ina jumla ya vuvuko 29 nchi nzima na boti ndogo nne ambazo zinasaidia kutoa katika vituo vichache ambavyo vina mahitaji kwa muda maalum kutokana na kupwa na kujaa kwa maji ambavyo ni Pangani-Mbweni, Kilambo-Namoto, Utete-Mkongo na Msangamkuu-Msemo.

Alisema katika kusimamia vivuko hivyo na boti, Serikali imebaini kuwapo na malalamiko kadhaa kutoka kwa abiria dhidi ya watumishi ambapo hudaiwa kutoa lugha zinazomkera mteja, kufanya kazi kwa mazoea, kutojali abiria, kupokea rushwa pale abiria anapofanya kosa likiwamo kupiga picha, kuharibu miundombinu, kutoshuka kwenye gari.

“Kule makao makuu kila siku tunapokea malalamiko kwa njia mbalimbali juu ya vitendo mnavyofanya sehemu za kazi, kwanza mnapokea fedha kutoka kwa abiria nje ya ofisi, kuwapiga abiria na hili linaelekezwa kwa askari wa Suma JKT, kuruhusu magari ya abiria yasiyokuwa na vibali kupita eneo la no entry, kuchelewesha kutoa huduma kwa mteja kutokana na kutokuwa na chenji.

“Naomba baada ya semina hii ya kukumbushana majukumu yetu, tubadilike kwa kutoa lugha nzuri kwa wateja, sikiliza malalamiko ya abiria, ukaribisho mzuri, toeni huduma bora ya hali ya juu ili vuvuko vya Serikali viwe kimbilio, mhudumie mteja ajione wathamani, jifunzeni kuomba msamaha pale inapotokea kuna kasoro na mwisho shukuru unapopokea fedha ya mtu kwa ajili ya huduma hiyo.

“Labda hamjajua kitu kimoja, unapotoa huduma bora kwa mteja ni tangazo kubwa na ni njia rahisi ya kukufanya ufanikiwe zaidi katika kutoa huduma, Serikali ambayo ina vitu vyote huduma yake haiwezi kufanana na watu binafsi lazima tuonyeshe utofauti,”alisema Bi Mbunda.

Hata hivyo, aliwataka askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) ambao wamepangiwa kazi kwenye vivuko vya Serikalai kupunguza amri pale wanapokuwa wanahudumia wateja. Aliongeza kuwa nguzo ya mafanikio ni kufanya kazi kama timu, hivyo watumishi wa TEMESA na askari hao wanapaswa kuwa kitu kimoja.

Naye Kapteni wa Kivuko cha Kuchelele-Ilunda, Ally Hassan, aliiomba Serikali kuboresha miundombinu kutoka Malimbe hadi kuvukoni kwa upande wa Mwanza, pia kutoka Ilunda hadi Sengerema kwa lengo la kuvutia wateja wenye magari ambao wanalazimika kuzunguka na kutumia vivuko vya Kamanga, Kigongo na Busisi.

Kapteni Hassan alisema ikiwa miundombinu hiyo itaboreshwa, kivuko hicho kitakuwa na wateja wengi sana kwani watakuwa wanatumia nusu saa kutoka upande wa Mwanza kwenda Wilaya ya Sengerema badala ya kuzunguka Kamanga, Kigongo na Busisi ambako wanatumia zaidi ya masaa mawili.

Naye Mkuu Msaidizi wa Kivuko cha Kigongo, Kashindi Hussein, alisema eneo lake lina wateja wengi kiasi cha kuzidiwa kutoa huduma ambapo gari ndogo, malori na mabasi yameendelea kuongezeka. Alisema licha ya ongezeko hilo lakini wameendelea kujitahidi kutoa huduma nzuri.

MWISHO