WAKAZI BUYAGU MBALIKA NA MAISOME NA KOME KUPATA VIVUKO VIPYA HIVI KARIBUNI

News Image

Posted On: August 15, 2024

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), inaendelea na ujenzi wa kivuko kipya kitakachokwenda kutoa huduma katika maeneo ya Buyagu na Mbalika Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ambacho ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 55%. Kivuko hicho kipya, kitakwenda kuunganisha Wilaya za Sengerema na Misungwi.

Serikali pia, inaendelea na ujenzi wa kivuko kingine kipya kitakachokwenda kutoa huduma kati ya eneo la Kome na Maisome kitakachokuwa na uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 kikiwana na tani 170, vivuko hivyo vinatarajiwa kupunguza adha ya usafiri wilayani Sengerema.

Akizungumza katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM mkoani Mwanza wilayani Sengerema Naibu Waziri Kasekenya amesema zaidi ya shilingi bilioni 73 zinatarajiwa kutumika kwenye ujenzi ili kuyaunganisha kwa barabara ya lami majimbo ya Sengerema na Buchosa na hivyo kuchochea shughuli za uvuvi, kilimo na biashara mkoani Mwanza.

Aidha Eng. Kasekenya amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Sengerema-Kamanga KM 32 kwa wilayani Sengerema ambayo ujenzi wake unakwenda kwa awamu.

Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema taratibu za kumpata mkandarasi mwingine ziko katika hatua za mwisho ili kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.5 mkoani Mwanza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Emmanuel Nchimbi ameipongeza Wizara ya ujenzi kwa kasi ya ujenzi wa daraja JP Magufuli Kigongo-Busisi lenye urefu wa Km 3 na barabara unganishi km 1.6 na kuzungumzia umuhimu wa kuweka alama zote za tahadhari katika daraja hilo kubwa nchini pindi litakapokamilika.

Amesisitiza umuhimu wa Wizara kuimarisha uwezo wa kuwapima vizuri wakandarasi kabla ya kuwapa mikataba ya miradi ili kuharakisha ujenzi wa miundombinu.

" Hakikisheni mnapata wakandarasi makini ili miradi ijengwe kwa wakati na ubora na hivyo kuleta tija kwa wananchi", amesisitiza Balozi, Dkt. Nchimbi.