TEMESA YASHUSHA NEEMA KWA WAKAZI WA KILWA KISIWANI NA LINDI KITUNDA

News Image

Posted On: July 28, 2021

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imeshusha neema kwa wakazi wa Kilwa Kisiwani na Lindi Kitunda baada ya leo kuwapelekea Boti mpya kwa ajili ya kubeba abiria na kubeba wagonjwa (Ambulance Boat).

Boti hizo mbili, MV. LINDI itakayotoa huduma ya kubeba abiria kati ya Lindi na Kitunda na MV. LUKILA itakayokuwa ikitoa huduma ya kubeba wagonjwa katika eneo la Kilwa Kisiwani, zote zimejengwa na kampuni za kizalendo kutoka Tanzania za Songoro Marine Transport Boatyard ya jijini Mwanza iliyojenga boti ya kubeba wagonjwa (Ambulance Fibre Boat) na kampuni ya Sam & Anzai Boat Builders Co. Ltd ya Dar Es Salaam iliyojenga boti ya abiria (Passenger Fibre Glass Boat) zimekabidhiwa rasmi leo katika hafla fupi iliyofanyika katika eneo la feri Mkoani Lindi mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Zainab Telack.

Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amesema kukamilika kwa boti hizo na kuanza kutumika kutaboresha huduma za afya kisiwani Kilwa pamoja na huduma za usafiri kwenye kivuko cha Lindi- Kitunda na maeneo mengine ambapo boti hizo zitapelekwa.

‘’Ninafurahi kusikia kuwa ununuzi wa boti hizi umefanyika kupitia bajeti ya Serikali kwa gharama ya shilingi za Kitanzania 99,710,000.00 kwa boti ya abiria na shilingi 217,600,000.00 kwa boti ya kubeba wagonjwa fedha yote ikiwa imetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’. Alisema Mhe. Telack ambapo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya ujenzi na Uchukuzi na Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA kwa kukamilisha ujenzi wa boti hizo.

‘‘Boti ya wagojwa ambayo naipokea leo itakabidhiwa kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Kilwa Kisiwani ambayo itakuwa na wajibu wa kusimamia uendeshaji wake na TEMESA itasaidia kutoa ushauri wa kitaalam na matengenezo kama inavyofanya kwenye kwenyemagari ya Serikali.‘‘ Aliongeza Mkuu wa Mkoa.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle, akisoma taarifa uhusu ujenzi wa boti hizo, amesema boti ya kubeba wagonjwa ina uwezo wa kubeba kilo elfu mbili (2000Kg) sawa na watu 12 kwa wakati mmoja. Boti hiyo pia ina sehemu ya muongozaji (Nahodha), sehemu ya kumuhudumia mgonjwa na sehemu ya kukaa wauguzi.

‘‘Boti hii ya wagonjwa pia ina vifaa maalum kwa ajili ya kumsaidia mgonjwa (Special equipment for medical rescue) kama vile Portable Oxygen system ikiwa na oxygen cylinder pamoja na regulators, humidifiers, masks na tubes.a Aidha, kuna Back Board yenye Head Immobilzer, Stethoscope za watu wazima na watoto, Portable Suction Unit pamoja na Kitanda cha kubebea mgonjwa (Stretcher).‘‘

‘‘Boti ya abiria nayo ina uwezo wa kubeba tani moja sawa na abiria 25 kwa wakati mmoja. Aidha, ina urefu wa mita 10, upana wa mita 2.5, kina mita 1.2 na kina cha kuelea (Draft) mita 0.5. Pia imefungwa injini mbili (Out board engine) aina ya SUZUKI ambazo uwezo wake ni “Horse Power” (HP) 30 kila moja. Inao uwezo wa kutembea kwa mwendokasi wa 12 Knots na itakuwa inaendeshwa kwa mfumo wa usukani (steering)’’. Alisema Mhandisi Maselle ambapo aliishukuru Serikali kwa ufadhili wa ujenzi wa boti hizi ambazo zitakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa Lindi (Lindi – Kitunda na Kilwa Kisiwani) kwani zitawaondolea adha ya usafiri waliyokuwa nayo hasa wakati wa dharura za wagonjwa.

Gharama zote za ujenzi wa boti hizo zimegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.