RC MTANDA AHIMIZA UKAMILISHWAJI KWA WAKATI MIRADI YA KIMKAKATI, AAHIDI USHIRIKIANO NA WAWEKEZAJI

News Image

Posted On: May 17, 2024

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda, Mei 16, 2024 amefanya ziara kukagua miradi ya kimkakati iliyopo wilayani Ilemela na kuhimiza ikamilike kwa wakati na kuahidi ushirikiano na mazingira mazuri kwa Wawekezaji. Mkuu huyo wa Mkoa akiwa ameambatana na uongozi wa Halmashauri ya Ilemela wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Hassan Masalla, amefika kwenye Karakana ya Songoro Marine inayojenga vivuko 5 vya Serikali vyenye gharama ya shs bilioni 28 vitakavyotoa huduma Wilaya za Magu, Ukerewe na Sengerema.

Mara baada ya kupatiwa taarifa fupi na Mkurugenzi wa kampuni hiyo Major Songoro iliyo muomba Mkuu huyo wa Mkoa kusaidia uharaka wa malipo, Mtanda ameahidi kuzungumza na Waziri wa Fedha na wa Waziri wa Ujenzi ili fedha ziletwe kwa wakati shs bilioni 8 hadi 10 ili zikamilishe miradi hiyo na wananchi wapate huduma bora na salama ya usafiri wa maji."Jana nimeshuhudia mwenyewe wakazi wa Ukerewe na Kisorya wanavyo taabika na shida ya usafiri kutokana na Kivuko cha MV. UJENZI kuwa na hitilafu ya injini na kuagiza Kivuko kutoka Sengerema kwenda kusaidia wananchi usafiri," Amesema Mtanda

Aidha ameipongeza Kampuni ya Songoro ambayo ni ya Kitanzania kwa kufanya kazi kizalendo licha ya changamoto ya uchelewashaji wa malipo lakini karibu kazi zote zipo hatua ya mwisho.

Mtanda amesema Serikali imeweka mazingira mazuri kwa Wawekezaji na bado Mwanza fursa za uwekezaji zipo nyingi Ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano wakati wote.