KAMISHNA WA TUME YA UTUMISHI WA UMMA ATEMBELEA TEMESA, ATOA PONGEZI KWA KUZINGATIA MAADILI NA UWAZI
Posted On: November 20, 2025
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umepokea ugeni kutoka Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ukiongozwa na Kamishna Bi. Suzan Mlawi, katika ziara maalum ya kikazi iliyofanyika makao makuu ya taasisi hiyo.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufanya tathmini ya namna watumishi wa TEMESA wanavyotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, uwajibikaji kazini, na uzingatiaji wa miongozo ya kiutumishi.
Akizungumza na menejimenti pamoja na watumishi wa TEMESA, Kamishna Mlawi alieleza kuwa ziara hiyo inalenga pia kufuatilia masuala ya upatikanaji wa mafunzo, utoaji wa likizo, upatikanaji wa vitendea kazi, pamoja na nidhamu kazini.
“Tunatoa pongezi kwa TEMESA kwa kudumisha maadili ya kazi, nidhamu na uwajibikaji. Ni matarajio yetu kuwa jitihada hizi zitaendelea kuboresha utendaji wa taasisi na kuongeza imani ya wananchi kwa huduma zenu,” alisema Kamishna Mlawi.
Ziara hiyo ilihusisha pia maafisa wengine wa PSC waliotoa wito kwa watumishi wa umma kuendelea kuwa waadilifu, wawazi na kuwajibika katika maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu waTEMESA, Lazaro Kilahala, aliwashukuru viongozi wa Tume kwa kutembelea taasisi hiyo na kuahidi kuwa TEMESA itaendelea kusimamia kwa nguvu misingi ya maadili ya kazi, uwajibikaji na kuzingatia sheria na taratibu za utumishi wa umma.