​MIRADI YA SHILINGI BILIONI 67 YATEKELEZWA NA TEMESA​

News Image

Posted On: May 13, 2024

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) wamekiri kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 67 ikiwa inajumuisha ujenzi na ukarabati wa karakana, ujenzi wa vivuko na maegesho ya vivuko.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala huo Bi. Josephine Matiro wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani Tarehe 10 Mei, 2024 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma jengo la Mkapa.

Matiro amesema kuwa Wakala unaendesha na kusimamia karakana 27 zilizopo katika Mikoa ya Tanzania Bara ambazo zinatoa huduma ya matengenezo ya magari, pikipiki, mitambo na kutoa huduma za ushauri na usimikaji wa mifumo ya Umeme na Viyoyozi katika majengo ya Serikali yaliyopo Tanzania Bara.

''Pamoja na kutekeleza majukumu yake ya msingi, Wakala unaendelea kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali yenye thamani ya shilingi Bilioni 67,723,669,720.20 naUSD 7,043765 ambayo inajumuisha ujenzi wa vivuko na maegesho, ukarabati wa vivuko na maegesho, ujenzi na ukarabati wa karakana na uanzishwaji wa karakana mpya katika Mikoa,'' amesema Matiro.

Aidha ameweka bayana kuwa Wakala upo mbioni kujenga karakana mpya na ya kisasa katika maeneo ya Kizota jijini Dodoma. ''Serikali imeweza kutoa zaidi ya shilingi Bilioni 7.2 ambazo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa karakana mpya na ukarabati. Mkoa wa Dodoma ni mojawapo ya mnufaika wa fedha hizo kwa kuwa Serikali kupitia TEMESA imeanza mchakato wa usanifu wa karakana mpya na ya kisasa ambayo itajengwa katika maeneo ya Kizota Mkoani Dodoma. Karakana hiyo inatarajiwa kuwa ya kisasa ambayo itaweza kuhudumia magari yote ya Taasisi za Serikali Mkoani Dodoma kwa ufanisi mkubwa,'' amebainisha Matiro.

TEMESA imetangaza mafanikio hayo ikiwa ni muendelezo wa Kipindi cha kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa Taasisi za Serikali Mkoani Dodoma kinachoratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa chini ya Kitengo cha Habari na Mawasiliano.