WAZIRI MKUU AAGIZA MAGARI YOTE YALIYOTELEKEZWA TEMESA KUFUFULIWA
Posted On: August 09, 2023
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kuhakikisha ifikapo Tarehe 30 mwezi Oktoba mwaka huu, magari yote ya Serikali yaliyoegeshwa katika karakana za TEMESA yawe yamefufuliwa na kuchukuliwa na Taasisi husika. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Tarehe 7 Agosti mwaka huu jijini Dodoma wakati alipokuwa akikabidhi magari na vifaa vya kupima afya kwa Idara ya Kazi na Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi (OSHA) ambapo amesema katika karakana za Wakala huo, yapo magari ambayo yameegeshwa kwa kipindi kirefu na kupelekea mengine kuharibika zaidi.
Waziri Mkuu ameuagiza pia Wakala kuboresha huduma, kuzingatia na kuongeza weledi katika kazi wakati wote kwakuwa Wakala huo unafanya kazi kubwa ya kusimamia matengenezo ya magari ya Serikali, Ameutaka pia Wakala kununua vipuri na vifaa vingine vya matengenzo ya magari ili huduma wanazotoa ziendelee kuwa bora.
''Kwahiyo TEMESA ngazi ya Mkoa, simamieni magari ya Serikali yaliyoko katika maeneo hayo, yanafanya kazi na yaendelee kufanya kazi, ifikapo Tarehe 30, Oktoba mwaka huu wa 2023, Taasisi zote zenye magari yaliyoegeshwa kwa muda mrefu huko TEMESA yawe yametengenezwa na kuondolewa na nipate Taarifa. Alisema Mhe. Kassim Majaliwa huku akiwataka maafisa usafiri kuzingatia mpango maalumu wa matengenezo ya magari hayo yawe yanafanyika kwa wakati, kuzingatia matumizi ya vifaa vyenye ubora na kutunza taarifa za kila gari kwakuwa hatua hiyo itapunguza idadi ya magari yanayowekwa kwenye maegesho kwa muda mrefu katika karakana za TEMESA ambayo hayatengenezwi na hayarudishwi kwenye Idara husika.