WAZIRI MKUU AZIAGIZA TAASISI ZINAZODAIWA NA TEMESA KULIPA MADENI

News Image

Posted On: August 21, 2024

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi zote zinazodaiwa na TEMESA kulipa madeni yao kwa haraka ili kuiwezesha kujiendesha kibiashara na kutoa huduma stahiki kwa wateja wake.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Agosti 20 wakati akifungua kongamano la tatu la madereva wa Serikali katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa AICC jijini Arusha ambapo amewataka TEMESA kuandika barua ofisini kwake kuainisha Taasisi zote zinazodaiwa ili kuandikiwa barua ya amri ya kuwalipa.

“Mtendaji Mkuu amekuja kulalamika hapa kwamba zipo taasisi zinadaiwa fedha nyingi sana, nilipokuja mwaka 2020 nilipata orodha ndefu na kuisimamia Wizara kulipa na fedha nyingi zililipwa, sasa nikuagize tena, lete tena orodha ya taasisi zote za serikali unazozidai ili tuziandikie barua (strong letter) ambayo inawataka kwa vipindi wawe wameshalipa maana hivi sasa hela wanazo kutokana na kuingiziwa katika mwaka huu wa fedha”, amesema Waziri Mkuu.

“Wakuu wa Taasisi popote walipo wananisikia, wapo humu ndani wako nje kupitia vyombo vya Habari walipe madeni yao TEMESA, ili TEMESA yetu itekeleze wajibu wa kuhakikisha vyombo vya usafiri vinakuwa salama na vinatengenezwa kwa wakati”, alisisitiza Waziri Mkuu.

Aidha Waziri Mkuu ameupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kwa kuwa na mitambo ya kisasa ya kutengeneza magari na kuwataka kuongeza ubunifu na uadilifu ili kuleta tija katika utengenezaji wa magari ya Serikali