RAIS SAMIA ATOA BILIONI 9 UJENZI KIVUKO KIPYA MAFIA-NYAMISATI
Posted On: September 30, 2024
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 9 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kipya kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Mafia Wilayani Mafia na Nyamisati Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Sept 28, 2024 wakati alipotembelea yadi ya DMG eneo la Kimbiji, Wilayani Kigamboni kukagua hatua za ujenzi wa kivuko hicho ambapo mpaka sasa kimefikia asilimia 35 za ujenzi wake.
Kunenge amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kuanza ujenzi wa kivuko hicho kwa wakazi wa Mafia na kutoa zaidi ya sh bilioni 9 kwa ajili ya utengenezaji wa kivuko hicho na pia amefarijika kwa hatua zilizofikiwa za ujenzi wa kivuko na kusisitiza umuhimu wake katika kukidhi mahitaji ya wananchi kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyohitajika.
"Awali, mradi ulitengewa bilioni 5, lakini kutokana na umuhimu wa kivuko hicho, Rais aliongeza fedha hadi kufikia zaidi ya bilioni 9 ili kuhakikisha kivuko kinajengwa kwa ubora unaohitajika," alisema Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
"Tumekuja kujua matengenezo yamefikia hatua gani na kuhakikisha ubora na viwango vinakidhi mahitaji ya wananchi," alisisitiza Mhe. Kunenge.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko kutoka TEMESA, Mhandisi Lukombe King’ombe, alisema kivuko hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 300, magari 10, na mizigo yenye uzito wa zaidi ya tani 120.
Naye Mbunge wa Mafia, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. Omary Kipanga, alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kivuko hicho, na kusisitiza umuhimu wa kivuko hicho kwa wananchi wa Mafia.
Kivuko cha Nyamisati-Mafia kitakapokamilika kitasaidia kutatua changamoto za usafirishaji kwa wananchi wa Mafia. Kivuko hicho kitakuwa na uwezo wa kusafiri kwa saa tatu kutoka Nyamisati hadi Mafia, pamoja na kuwa na huduma kama sehemu ya kusafirishia maiti, huduma ya kwanza, vyoo, sehemu ya kuhifadhia mizigo ya abiria, na eneo la kulia chakula.
Kivuko hicho kipya kinachojengwa na kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG), kitakwenda kukiongezea nguvu kivuko MV. KILINDONI ambacho kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari madogo 10 kikiwa na tani 100.