“RAIS DKT.SAMIA ANAFANYA KILA JITIHADA KUWALIPA WAKANDARASI WAZAWA,” ULEGA

News Image

Posted On: January 29, 2025

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amewatoa hofu wakazi wa Buyagu Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza na kuwataka wawe wavumilivu kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kila jitihada kuhakikisha anawalipa wakandarasi wa ndani ili kazi za ujenzi wa maegesho ya vivuko na miundombinu yake ikiwemo majengo ya kupumzikia abiria, vyoo, ujenzi wa kivuko kipya kitakachotoa huduma kati ya Buyagu na Mbalika pamoja na barabara ambayo itakuwa ikielekea eneo kivuko kinaposinama kushusha abiria ziweze kufanyika na kukamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma stahiki.

Waziri Ulega ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara ya kikazi katika eneo la Buyagu, wilayani Sengerema, mkoa wa Mwanza, ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya cha Buyagu Mbalika ambacho ujenzi wake unaendelea katika Yadi ya Songoro, alikagua pia ujenzi wa maegesho ya kivuko ambao unaendelea katika eneo la Buyagu amabo mpaka sasa umefikia zaidi ya Asilimia 15 pamoja na kuongea na wananchi wa eneo hilo ambapo alisisitiza umuhimu wa kukamilika kwa miradi ya vivuko na barabara huku akitoa maagizo mahsusi kwa viongozi wa Taasisi husika.

Waziri Ulega alisema ujenzi wa kivuko hicho ni kazi kubwa muhimu sana kwa shughuli za usafiri wa majini katika eneo hilo, lakini pia aliweka msisitizo kuwa wakati wakisubiri kivuko hicho kikamilike, usafiri wa barabara ni muhimu pamoja na eneo la kupumzika kwa wakazi wa Buyagu na mkoa wa Mwanza kwa ujumla na serikali itahakikisha inatekeleza miradi ya miundombinu kwa ufanisi na kwa haraka ili kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.

“Hii ni kazi kubwa sana na ni kazi iliyotukuka, vile vivuko ni vikubwa leo nimevikagua na vimeniridhisha tunachosubiri tu ni ukamilifu wa vifaa, vifaa vinaingizwa kwenye meli na kusafirishwa mpaka vifike hapa kwa hivyo ni kitu cha kusubiri lakini kwa kazi ambazo zimekwisha fanyika hamna sababu tena ya kukosa imani kazi iliyobaki ni kukamilisha na muanze kukitumia mahala hapa” alisisitiza Waziri wa Ujenzi

“Mbunge wenu wa Sengerema Mhe.Tabasamu mara ya kwanza alimuomba Mhe.Rais Samia na Rais Samia ameridhia, tunajenga hicho kivuko, tunajenga na kivuko kingine Nyakarilo Kwenda Kome sasa hii ni kazi kubwa n ani kazi iliyotukuka”, aliongeza Mhe.Ulega.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mtendaji Mkuu Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala amesema ujenzi wa maegesho ya kivuko pamoja na barabara umefikia asilimia 15 na mpaka kufikia mwezi wa watatu ujenzi utakuwa umeshakamilika.

Naye Mbunge wa jimbo la Sengerema Mhe. Hamisi Tabasamu ameelezea furaha ya wananchi wake kwa kupata kipaumbele cha miradi ya ujenzi wa vivuko, maegesho na barabara na kuwapongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) na Wizara ya Ujenzi kwa kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa wakati ili wananchi wa Sengerema na maeneo jirani waweze kunufaika na miundombinu bora ya vivuko na barabara.