UTARATIBU WA MALIPO KABLA (PREPAID) KULIPIA HUDUMA ZA MATENGENEZO ZINAZOTOLEWA NA TEMESA WAANZA KUTUMIKA RASMI

News Image

Posted On: March 03, 2025

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kupitia ofisi zake zote Nchini umeanza kutumia utaratibu mpya wa kulipia malipo kabla ya huduma (Prepaid) ili kuboresha utendaji kazi wake ambapo mteja sasa anaehitaji huduma za matengenezo ya magari, pikipiki, mitambo, makangavuke (majenereta), viyoyozi, huduma za TEHAMA na kazi za umeme na elektroniki atahitajika kulipia kabla ya kupatiwa huduma hizo.

Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro Kilahala wakati alipokuwa akitoa taarifa hiyo mapema leo mjini Dodoma ambapo amesema kwa muda mrefu hali ya utendajikazi wa Wakala huo ilikuwa isiyoridhisha kutokana na Taasisi kushindwa kuyaishi makusudi makuu ya kuanzishwa kwake ambayo ni kulinda usalama wa viongozi na Watumishi wa Umma kupitia matengenezo thabiti ya magari, mitambo, mifumo ya umeme na elektroniki, kuzuia upotevu wa fedha za Serikali kwa kuhakikisha matengenezo hayo yanafanyika kwa gharama sahihi lakini kutokana na baadhi ya Taasisi na Wizara kushindwa kulipia huduma hizo kwa wakati,

Kilahala amesema, Wakala ulijikuta ukiingia katika madeni makubwa ambayo yakasababisha ushindwe kutoa huduma zake kwa ufanisi mkubwa.Kufuatia hali hiyo, Serikali iliiagiza Wizara ya Ujenzi kuandaa Mkakati Madhubuti wa kuifufua TEMESA. Baada ya kufanya utafiti wa kina, ilibainika kuwa tatizo la msingi linalozorotesha utendajikazi wa TEMESA ni ukosefu wa fedha kutokana na hudumaza matengenezo zinazotolewa na TEMESA kulipiwa kwa utaratibu wa malipo baada (Postpaid) jambo lililopelekea uwepo wa madeni makubwa ya kudai ambayo yalifikia zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni 66 na kudaiwa shilingi Bilioni 61 mpaka kufikia Tarehe 30 Julai 2024.

Itakumbukwa kwamba utaratibu kama huo ndio ulipelekea kuzorota kwa utendajikazi wa taasisi kama vile Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Kuthibiti Ununuzi wa Umma Tanzania (PPRA), Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA)na nyinginezonyingi mpaka hapo zilipohamia katika utaratibu wa malipokabla (Prepaid).


Hali hiyo ya ukata wa muda mrefu ilipelekea TEMESA kushindwa kuajiri, kutunza (retain)na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa mafundi wake, kubambikiwa bei zajuu za vipuri na Wagavi wasio waaminifu kutokana na madeni makubwa wanayoidai Taasisi pamoja na kuuziwa vipuri visivyo na ubora, kupungua kwa Uadilifu na ari ya utendajikaziwa baadhi ya watumishi wa TEMESA, kushindwa kujinunulia vitendea kazi vya kisasa na kuboresha mazingira ya utendajikazi, pamoja na madhila mengine kadha wa kadha.

Kufuatia kadhia hiyo, mkakati madhubuti uliandaliwa na kuwasilishwa kwa mamlaka ukipendekeza mabadiliko kadhaa katika mfumo wa utendajikazi wa TEMESA ikiwemo kuruhusu kuanza kutumika kwa utaratibu wa malipo kabla kwa huduma za matengenezo zinazotolewa na TEMESA, wadaiwa wote kulipa madeni yao ifikapo tarehe 30 Juni, 2025 na TEMESA kulipa wadeni wake wote ifikapo tarehe 01 Julai, 2025, TEMESA kufanya mapinduzi makubwa katika ubora wa huduma za ufundi kwa kuajiri mafundi wazuri popotewalipo, kuwapa mafunzo ya mara kwa mara na motisha, TEMESA kuandaa utaratibu wa kuanza kuagiza vipuri kwa wingi moja kwa moja toka kwa wazalishaji au Mawakala wao pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa karakana zake.

Kufuatia maombi hayo, mamlaka iliridhia mabadiliko haya na kuagiza yatekelezwe kuanzia tarehe 01 Januari 2025 na hivyo Wakala umeanza rasmi kutumia utaratibu wa malipo kabla (Prepaid) kwa huduma za matengenezo zınazotolewa na TEMESA pamoja na mabadiliko mengine kama yalivyoainishwa.