KATIBU MKUU UJENZI AITAKA TEMESA KURUDISHA IMANI KWA WATEJA

News Image

Posted On: June 04, 2021

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Joseph K. Malongo ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kuhakikisha unakuja na mkakati maalumu ili kurudisha imani ya wateja ambao ni watumiaji wa huduma za Wakala huo ambao ni taasisi za Serikali na Umma.

Mhandisi Malongo ameyasema hayo mapema leo wakati akizindua rasmi vitendea kazi vipya vya karakana na viti maalumu vya walemavu katika hafla fupi iliyofanyika katika karakana ya TEMESA Mkoa wa Dodoma.

Wakala umenunua Viti Maalum vya Walemavu thelathini na tatu (33) kwa ajili ya kusaidia abiria walemavu wanaovuka katika Vivuko vya Serikali. Vifaa hivi vimegharimu Serikali kiasi cha Tsh 765,512,400 kati ya fedha hizi kiasi cha Tsh 494,814,900 zimetumika kununua Karakana zinazohamishika, Tsh 257,205,780 zimegharamia manunuzi ya Diagnostic Machine na Sinograph na Tsh 13,491,720 Viti Maalum vya Walemavu.

‘’Tunatakiwa tuje na mkakati maalumu, ‘Turn around strategy’, masoko tunayo, uhakika wa soko tunao ambao umehakikishwa na sheria inayotulinda, magari na mitambo elfu kumi na tano watoa huduma wengine hawana, lakini nyie mnayo, njoeni na mkakati tuangalie tunawezaje kurudisha Imani ya wateja wetu na wateja wetu ni Serikali’’.

Alisema Mhandisi Malongo ambapo aliongeza kuwa mkakati huo ndio utakaoonyesha njia ambayo Wakala huo utaelekea mara baada ya kuutekeleza kwa usahihi.

‘’Niwapongeze kwa hatua nzuri ya kwanza ya kusogeza huduma karibu na wateja wetu, na nimatumaini yangu kwamba vifaa hivi ambavyo vimenunuliwa kwa pesa nyingi za serikali vitaenda kutumika vizuri kwa mahala husika’’. Alimaliza Katibu Mkuu.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y.Maselle amesema ununuzi wa karakana zinazohamishika (Mobile Workshops) umelenga kusogeza huduma kwa wateja waliombali na karakana za Mikoa na pili ni kutoa huduma ya matengenezo ya dharura yanayotokea maeneo yasiyo na karakana hasa magari na mitambo yanapokuwa safarini au kazini nje ya ofisi.

Aidha aliongeza kuwa karakana za Wilaya zilizombali na karakana za Mikoa zitaendelea kujengwa kadri ya upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na Karakana zinazohamishika.

Mhandisi Maselle amesema kuwa Vifaa vya kuchunguza ubovu na hitalafu za magari na mitambo (Diagnostic Machines) viko therasini (30) kwa lengo la kila kituo kuwa na machine yake.

‘’Wakala unaamini kubaini tatizo kwa usahihi na kwa muda mfupi kutaboresha ubora wa huduma na kupunguza muda wa matengenezo ya magari na mitambo. Vilevile katika kupunguza malalamiko ya wateja kufungiwa vipuri visivyo halisia, Wakala umenunua viweka alama kwenye vipuri (Sinograph) vitakavyotumika kwenye matengenezo ya magari na mitambo katika karakana za TEMESA zote’’.

Karakana hizi zinazotembea zitagawiwa katika Mikoa ya kikanda; Mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Mbeya, Tabora na Dodoma. Katika mwaka wa fedha 2021/22, Wizara kupitia Wakala imetenga fedha kwa ajili ya kununua Karakana za aina hii zingine sita (6).