KATIBU MKUU UJENZI ATOA MELEKEZO KIVUKO CHA MV TANGA: ‘NIPATE TAARIFA KILA SIKU’
Posted On: August 12, 2025
Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, ametoa maelekezo kwa Meneja wa Kivuko cha MV. Tanga kinachotoa huduma kati ya Pangani na Bweni mkoani Tanga kuhakikisha anawasilisha taarifa ya utendaji kazi wa kivuko hicho kila siku ifikapo saa Tatu asubuhi.
Maelekezo hayo ameyatoa alipokuwa ziarani mkoani Tanga baada ya kutembelea kivuko hicho ambapo amesema kuwa amekuwa akipokea taarifa za hitilafu za kivuko hicho mara kwa mara pamojana malalamiko kutoka kwa wananchi kutokana na kutokutoa huduma za kuridhisha.
“Nataka nipate taarifa za kivuko kila siku saa Tatu, Meneja ndiye utakayenitumia taarifa hiyo ikionesha kivuko hicho kimefanya idadi ya safari ngapi kwa siku na kama ndizo zinazotakiwa kwa siku au la”, amesema Katibu Mkuu.
Aidha, Balozi Amour ameelekeza taarifa hiyo ieleze sababu ya hitilafu husika endapo kivuko hicho kitakuwa na changamoto yoyote na pia ieleze huduma hiyo imesimama kwa muda gani pamoja na hatua zilizochukuliwa kutatua changamoto hizo.
Katibu Mkuu ameelekeza pia Mkuu wa Kanda ya Mashariki na Kusini Abdulrahman Ameir wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ahakikishe anaweka kambi Pangani ili kufuatilia kwa karibu utendaji kazi wa kivuko hicho hadi hapo Daraja litakapokamilika.
"Sasa navunja huo utaratibu wenu, Meneja wa mkoa wa Tanga utatakiwa ujue kila kinachoendelea kwenye hiki kivuko, taarifa utapata kupitia kwa msimamizi wa kivuko na Meneja wa Kanda aje apige kambi hapa", ameongeza Katibu Mkuu.
Katika hatua nyingine, Balozi Amour ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Daraja la Pangani ambapo ameonesha kutokuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kumtaka mkandarasi Shandong Luqiao Group kuongeza kasi ya Ujenzi ili kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa.
Amefafanua kuwa Mkandarasi wa mradi huo anapaswa kukamilisha Daraja hilo ifikapo Desemba, 2025 na kueleza kuwa hadi sasa amefika asilimia 69 tu huku akiwa amebakisha miezi michache kukamilisha kazi hiyo kulingana na mkataba.
Ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 na Barabara unganishi(Km 25) unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.