MKUU WA WILAYA YA KILWA ATEMBELEA BANDA LA TEMESA, APATA ELIMU KUHUSU MAGEUZI YA KITEKNOLOJIA

News Image

Posted On: August 08, 2025

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, ametembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi, na kupata maelezo ya kina kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo.

Akizungumza na Meneja wa TEMESA mkoa wa Lindi, Mhandisi Jamali Waziri, Mhe. Nyundo amepewa ufafanuzi kuhusu mikakati ya maboresho inayoendelea ndani ya TEMESA, hususan matumizi ya teknolojia kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM) unaolenga kuongeza uwazi, ufanisi na ufuatiliaji wa huduma kwa vyombo vya serikali.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amepongeza juhudi zinazofanywa na TEMESA katika kuboresha huduma kwa kutumia vifaa vya kisasa.

TEMESA inatoa wito kwa wananchi na wadau wote kutembelea banda lao katika maonesho hayo ili kupata elimu zaidi kuhusu huduma wanazotoa na namna ya kushirikiana katika uboreshaji wa miundombinu ya serikali.