KATIBU MKUU MWAKALINGA AIAGIZA TEMESA KUTUNZA NA KUHESHIMU RASILIMALI WATU
Posted On: September 11, 2020
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius A. Mwakalinga ameutaka Wakala huo kutumia Baraza la Wafanyakazi kuhakikisha wanashirikisha watumishi katika masuala yanayohusu mustakabali wa Wakala huo ikiwemo utoaji wa maamuzi ili kuweka dhana ya umoja katika utendaji wa kazi.
Arch. Mwakalinga ameyasema hayo leo wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ufundi (VETA) mjini Dodoma ambapo pamoja na hayo aliitaka TEMESA kuhakikisha inachagiza maelewano, uhusiano na ushirikiano baina ya watumishi na kuzingatia maadili ya watumishi wa Umma.
“Fedha ni rasilimali lakini sio watu, fedha ukiiacha hapo leo kesho utaikuta hapo hapo, lakini rasilimali watu ndiye anayeitunza hiyo fedha rasilimali watu ndiye anayetengeneza kivuko, ndiye anayeenda kuweka sawa mifumo ya umeme.” Alisema Arch. Mwakalinga na kuongeza kuwa rasilimali watu ndiyo inayosababisha taasisi kuweza kujiendesha kwa ubunifu na uwajibikaji ili kuhakikisha taasisi inaenda mbele hivyo rasilimali watu inapaswa kuheshimiwa na kutunzwa.
Aliuagiza Wakala pia kuhakikisha wanarudi nyuma na kuangalia majadiliano na makubaliano waliyofikia kwenye vikao vya Baraza viliyopita na kuyafanyia kazi ili kuona wametekeleza yapi na kuyashindwa yapi na kwasababu zipi na kama bado yapo na yanatekelezeka au hayatekelezeki.
“Kila mwaka tutakuwa tukiandikiana barua kwamba hili limepelekwa mbele, hili tulikamilisha, baada ya hapo tunakuwa tumefunga mjadala wa yale ambayo tulielekezana”. Alisisitiza Katibu Mkuu na kuongeza kuwa majadiliano hayo yawe ni kwa ajili ya kubaini mapungufu, changamoto na uwezo wa Wakala katika kutekeleza majukumu yake ya msingi.
Awali akisoma taarifa fupi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle aliiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuunda mfuko maalumu ili kuondokana na mzigo mkubwa wa madeni unaoukabili Wakala ambao unadhoofisha juhudi za TEMESA katika kutekeleza majukumu yake.
“Tunaiomba serikali iangalie uwezakano wa kuunda mfuko wa kuhudumia matengenezo ya magari yake kama ilivyokuwa zamani wakati wa mfuko wa kuhudumia Mitambo ya Serikali (PTMF)”. Alisema Mhandisi Maselle.
Mtendaji Mkuu pia aliomba kuanzishwa kwa utaratibu wa ununuzi wa vipuri moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wa magari kwa kushirikiana na Wakala ya Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) ambao ndio waliokasimishwa kufanya ununuzi wa pamoja wa magari ya Serikali ambapo alisema utaratibu huo utawahakikishia upatikanaji wa vipuri halisi na kwa bei halisi na hivyo utapunguza gharama ya matengenezo ya magari ya Serikali.