MV. MWANZA YAANZA RASMI KUTOA HUDUMA NYAKALIRO KOME
Posted On: July 04, 2025
Kivuko cha MV. MWANZA kilichokuwa kinatoa huduma kati ya Kigongo Wilayani Misungwi na Busisi Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza kimewasili rasmi katika eneo la Nyakaliro na Kome Halmashauri ya Mji Buchosa Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza kuanza rasmi kutoa huduma katika eneo hilo baada ya kuhamishwa kutoka eneo la Kigongo Busisi ambako kilikuwa kinatoa huduma hapo awali.
Kivuko MV. MWANZA chenye uwezo wa kubeba abiria 1000, magari 36, kitakuwa kikitoa huduma eneo hilo kwa kusaidiana na kivuko MV. KOME II ambacho kinao uwezo wa kubeba abiria 100 kikiwa na tani 40.
Kivuko hicho pamoja na vivuko vingine viwili MV. MISUNGWI na MV. SENGEREMA, vilisimama rasmi kutoa huduma eneo la Kigongo Busisi baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua rasmi Daraja la JP . MAGUFULI siku ya Tarehe 19 Juni, 2025.
Daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3 na barabara unganishi kilometa 1.6, linaunganisha Mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani na tayari lieonekana kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa Mikoa hiyo na nchi jirani.