KATIBU MKUU UJENZI AITAKA TEMESA KUBORESHA HUDUMA ZAKE NA KULINDA MAPATO
Posted On: February 02, 2022
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Balozi Mhandisi Aisha S. Amour leo amefanya kikao na menejimenti na mameneja wa Mikoa na vituo vya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na kuwataka watumishi wa Wakala huo kuwajibika katika kutimiza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi na kulinda mapato. Katibu Mkuu amezungumza hayo leo wakati wa kikao kilichofanyika katika ukumbi wa VETA Dodoma ambapo amewaagiza mameneja wa Mikoa na vituo kuhakikisha wanaboresha mazingira ya kazi katika vituo vyao, wanalinda vyanzo vya mapato na kutumia fedha za Serikali kwa uwazi huku wakihakikisha kila mtumishi anawajibika katika majukumu yake ya kila siku.
''Tutaboresha huduma zote kwa kuweka mifumo ya kisasa ili kupunguza mianya ya wizi, dhumuni letu ni kuangalia ni jinsi gani tutaboresha huduma na kupunguza gharama za uendeshaji''. Amesema Balozi Aisha S. Amour
Akiongelea kuhusu madeni ambayo Wakala huo unadai kwa Taasisi mbalimbali za Umma, Mhe. Balozi Aisha Amour amesema Wizara itahakikisha wadaiwa sugu wote wanalipa madeni yao ili Wakala uweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
‘’Tunajua kwamba mna matatizo mengi, yote tumeyapokea, hasa hayo ya wadaiwa sugu, hilo tutashirikiana kuhakikisha kwamba wote wanaodaiwa wanalipa madeni yao’’. Alimaliza Balozi Aisha huku akiwataka TEMESA kujipanga kuboresha huduma zake kwa kuangalia changamoto zote na kuzifanyia kazi kwa wakati.
Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro N. Kilahala akizungumza katika kikao hicho amesema Wakala umejivunia mafanikio katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuongeza uzalishaji kutoka shilingi bilioni 4.3 kwa mwaka wa fedha 2006/7 hadi kufikia shilingi bilioni 59.5 kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Mtendaji Mkuu pia alitoa mapendekezo ambapo aliiomba Serikali itoe maelekezo kwa Wizara na Taasisi zake kulipa Wakala kabla ya kuchukua magari yaliyotengenezwa au malipo hayo yafanyike moja kwa moja Hazina.
Aidha kwa upande wa vivuko, Mtendaji Mkuu aliiomba Serikali iridhie kuongeza nauli za vivuko hasa kwa mizigo, magari na vyombo vya moto ili kuimarisha mapato ya vivuko na kuimarisha huduma ambapo nauli hizo mara ya mwisho zilipandishwa Zaidi ya miaka 10 iliyopita.
‘’Serikali iridhie kupunguza baadhi ya majukumu ya Wakala ili Wakala ujikite katika kuyafanya majukumu ya msingi kwa ufanisi na tija zaidi. Alimaliza Lazaro N. Kilahala.